Tanzania kuendelea kutoa ruzuku kwenye mafuta hadi bidhaa hiyo itakaposhuka bei

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kukata matumizi yake kila mwezi na kutoa ruzuku ya mafuta hadi pale bei itakapokuwa sawa katika soko la dunia. 

Serikali ilianza kutoka zuruku ya shilingi bilioni 100 mwezi huu na kuleta ahueni kwenye bei za nishati ya mafuta ambapo Petroli ilipungua kwa shilingi 152 hadi 306 na dizeli shilingi 320 hadi 488 kutegemeana na eneo.

Ruzuku hiyo iliyoanza kutumika tarehe 1 Juni, 2022, ilipunguza bei za mafuta ya petroli kutoka shilingi 3,301 hadi 2,994 na dizeli kutoka 3,452 hadi 3,131 kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza na wananchi wa Bwanga mkoani Geita akielekea mkoani Kagera, leo Jumatano tarehe 8 Juni, 2022, Rais Samia amesema, “tunajaribu kutoa ruzuku kama mlisikia mwezi uliopita nilisema nitatoa shilingi bilioni 100 ili bei zishuke na mwezi huu bei zimeshuka tutaendelea kutoa hiyo ruzuku hadi dunia ikae sawa tutaendelea kukata matumizi ya Serikali kutoa ruzuku mpaka bei zikae sawa.”

Amesema jitihada zingine Serikali inayofanya ni kuziambia nchi zinazopigana (Urusi na Ukreani) kuacha mapigano ili mambo yawe sawa.

“Tunachokifanya ili kupunguza makali dunia nzima tunaziambia zile nchi mbili ziache kupigana kwasababu zikiacha kupigana tunapata manufaa mengi tu,amesema Rais Samia.

Akifafanua kwa wananchi namna vita hiyo inavyoathiri upandaji wa bei za bidhaa Rais Samia amesema moja ya nchi iliyokuwa inategemewa kwa gesi katika Mataifa ya Magharibi ipo vitani na hivyo kusababisha nchi hizo kugeukia mafuta.

Ameeleza zaidi kuwa hali hiyo imesababisha kuwepo mahitaji makubw aya mafuta na kusababisha bei kupanda kwa kasi.

Mkuu huyo wa nchi ameendelea kueleza kuwa bei kubwa ya mafuta imesababisha kuongezeka kwa gharama ya kusafirisha bidhaa ambapo amesema kontena lilikuwa likisafirishwa kwa dola 1,800 hivi sasa linasafirshwa kwa dola 8,000 hadi 9,000.

“Lakini mafuta yanavyopanda yakifika hapa kwetu mwenye gari ananunua kwa bei kubwa kwahiyo na yeye anarudisha kwenye nauli hata bodaboda mmenunua mafuta na mmepandisha bei,” amesema.

Rais Samia yupo mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu ambapo ziara hiyo imeanza leo na inatarajiwa kuhitishwa keshokutwa.