Serikali ya Tanzania imesema inafatilia kwa ukaribu makala mpya ya televisheni ya kimataifa ya CNN, ambayo imeeleza kwa kina madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na matukio ya vifo vya watu wakati wa maandamano yaliyofuatia uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Katika makala hiyo, CNN iliripoti kuwepo kwa kaburi la pamoja katika makaburi ya Kondo jijini Dar es Salaam, ikidai kuwa miili ya waandamanaji waliouawa na vyombo vya dola ilizikwa kwa siri. Uchunguzi wa chombo hicho cha habari pia ulionyesha picha za satelaiti zinazoashiria udongo uliovurugika, ushuhuda wa madaktari waliotibu majeruhi wa risasi, pamoja na video na picha zinazowaonyesha raia waliouawa katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, CNN iliripoti kuwa idadi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko inavyotangazwa, huku upinzani ukikadiria kuwa zaidi ya watu 2,000 waliuawa katika wiki ya maandamano. Hospitali kadhaa zimeripotiwa kufurika miili ya waathiriwa wa vurugu hizo, athari ambazo zimelaaniwa vikali na watetezi wa haki za binadamu.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imesema bado inaendelea kuchambua yaliyomo katika makala hiyo kabla ya kutoa msimamo wake rasmi.
Akizungumza katika taarifa fupi kupitia mitandao ya kijamii, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema
“Serikali imefuatilia makala iliyochapishwa muda mfupi uliopita na chombo cha habari cha CNN kuhusu matukio ya tarehe 29, 2025 na siku zilizofuata. Tunachambua na kuhakiki maudhui yaliyomo katika makala hiyo na tamko la Serikali litakuja baada ya kukamilika kwa uhakiki huo.”
Mpaka sasa, Serikali haijatoa takwimu kamili za watu waliouawa au kujeruhiwa wakati wa machafuko hayo, huku kukiwa na miito kutoka kwa jumuiya za haki za binadamu na viongozi wa dini kuitaka serikali kuweka uwazi na kutoa majibu ya kina kuhusu tuhuma hizo.
Serikali inatarajiwa kutoa taarifa kamili pindi uchambuzi wa makala ya CNN utakapokamilika.