Serikali ya Tanzania imejipanga kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa Maliasili na Utalii nchini humo, Balozi Pindi Chana alisema hayo jana jijini Arusha wakati akifungua kikao cha wadau wa utalii kujadili changamoto na kutoa ushauri ili kuboresha mazingira ya sekta hiyo.
Chana alisema kikao hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Juni 7 mwaka huu.
Alisema Rais Samia aliagiza wizara hiyo ikutane na wadau wa sekta ya utalii ili kujadili mapendekezo ya mageuzi ya sera, sheria taratibu na kanuni kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta hiyo.
Chana alisema wizara imedhamiria kuboresha mazingira ya uwekezaji biashara katika sekta ya utalii, ikiwemo kupunguza wingi wa usajili, tozo mbalimbali na malipo ya ada ya leseni.
Pia alimpongeza Rais Samia kwa kutengeneza Filamu ya Royal Tour ambayo kwa sasa imeanza kuonyesha matunda kwa kupokea idadi kubwa ya watalii na kuleta matumaini kwa sekta hiyo.
Alisema kupitia kikao hicho wanatarajia kupokea mawazo, ushauri na mapendekezo pamoja na njia ya kuzitatua ili kuleta matokeo changa katika sekta hiyo.
Mshauri wa Mazingira ya Uwekezaji kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa, Anita Kundy alisema IFC ni miongoni mwa waliotoa msaada wa kikundi kuunga mkono utayarishaji wa marekebisho ya sera na ripoti ya masuala ya jinsia ambayo ni nguzo kuu katika kikao hicho.
Alisema ripoti hiyo iliandaliwa na sekta binafsi kupitia mashauriano ya kina na vyama vyote vya utalii nchini kwa msaada wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).