Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, imejipanga kurejea upya gharama za upandikizaji wa mimba kwa wananchi wenye matatizo ya uzazi na kutopata watoto, ili kuwapunguzia mzigo wa gharama kubwa endapo watajiunga na bima ya afya kwa wote.
Kauli hiyo imetolewa jana mara baada Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutembelea taasisi ya Hospitali ya Kairuki iliyopo Bunju A jijini Dar es Salaam, ambayo inatoa huduma ya upandikizaji mimba kwa lengo la kuona huduma zinazotolewa kituoni hapo.
Ummy amesema tatizo la ugumba nchini Tanzania bado ni kubwa, lakini mpaka sasa hakuna takwimu rasmi za kitaifa, ila ulifanyika utafiti mdogo ambao unaonesha asilimia 30 ya watu wana tatizo la ugumba, huku duniani inakadiriwa kuwa katika kila mahusiano ya wenza wanne, mmoja kati yao anakua na tatizo la kupata watoto.
“Tatizo la kutopata watoto lipo pande zote mbili, upande wa wanaume na wanawake, lakini jamii yetu inachukulia familia isipopata mtoto basi mwanamke ndiyo anaonekana mwenye tatizo. Naamini uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa fikra potofu,” amesema Waziri Ummy.
Kituo cha upandikizaji mimba cha Kairuki kinatoa huduma hiyo kwa gharama ya kuanzia shilingi milioni 13 hadi shilingi milioni 17 kutegemea na aina ya huduma inayohitajika, hata hivyo Waziri Ummy amesema serikali itaangalia uwezekano wa kuweka nusu ya gharama hizo katika vifurushi vya bima ya afya kwa wote, ili kuwapunguzia wananchi gharama za kupata huduma hiyo.
“Sisi upande wa Serikali tutaendelea kuwaunga mkono na kuhakikisha kwamba huduma hizi zinatolewa na kuwafikia wengi, tumeelezwa hapa gharama za upandikizaji ni kubwa Watanzania wengi hawawezi kumudu.
“Kwa hiyo nashukuru mmenileta kipindi hiki tunaenda kuwasilisha muswada wa bima ya afya kwa wote bungeni kwa hiyo nitaangalia uwezekano wa bima kuweza kugharamia asilimia 30 au 40 ya baadhi ya huduma zinazohitajika,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ametoa pongezi kwa taasisi ya Kairuki kwa kujenga kituo hicho na kuongeza kuwa ni muhimu sana uwepo wake nchini, kwani kitamsaidia Mtanzania kupata huduma za upandikizaji wa mimba ndani ya nchi, hivyo amewasisitiza wananchi kwenda kituoni hapo kupata huduma badala ya kutumia fedha nyingi kwenda nje ya nchi.