Search
Close this search box.
Africa

Wizara ya Afya nchini Tanzania inatarajia kuanza Kampeni ya Awamu ya tatu ya kutoa matone ya chanjo ya Polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kuanzia Septemba 1 hadi 4 Mwaka huu 2022.

Waziri wa Afya nchini humo Ummy Mwalimu amesema utoaji wa chanjo hiyo ni kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo uliotokea katika nchi jirani ya Malawi mnamo Februari 17, 2022 na kisha nchini Msumbiji mnamo Mwezi Mei 2022.

“Sasa tunaelekea kufanya Awamu ya tatu ya Kampeni ya kutoa chanjo ya matone ya Polio ambayo itaanza terehe 1 hadi 4 Septemba, 2022 na zoezi hili litakuwa nchi nzima” amesema Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amesema kuwa zoezi hilo la utoaji wa matone ya Chanjo ya Polio litafanyika nchi nzima huku kwa Awamu hii ya tatu wakiwa wamelenga kuwafikia watoto 12,386,854 walio chini ya umri wa miaka mitano.

“Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza kuwa unapotokea mlipuko au tishio la mlipuko wa Ugonjwa wa Polio nchini, nchi husika na nchi Jirani zipaswa kufanya Kampeni ya kutoa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa awamu nne mfulilo” amesema Waziri Ummy Mwalimu akifafanua kwa nini zoezi la Chanjo hilo limekuwa likirudiwa mara nyingi.

Waziri Ummy amesema kuwa Kampeni mbili za awali za utoaji wa matone ya Chanjo ya Polio lilikuwa na mafanikio makubwa kwa kufanikisha chanjo hiyo kwa watoto wengi zaidi na kuwataka Wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam wa afya katika zoezi hili awamu ya tatu.

“Awamu ya kwanza ya kampeni ilifanyika kuanzia tarehe 24 hadi 27 Machi 2022 na ilitekelezwa katika Mikoa minne inayopakana na nchi ya Malawi ambayo ni Mbeya, Songwe, Ruvuma na Njombe na kufanikiwa kuchanja watoto 1,130,261 sawa na asilimia 115 ya watoto walio chini ya miaka mitano” amesema Waziri Ummy 

Awamu ya pili ya utoaji wa chanjo ya polio  ilifanyika nchi nzima kuanzia tarehe 18 hadi 21 Mei 2022 na kuwafikia watoto 12,131,049 sawa na asilimia 118.8.

Waziri Ummy amewasihi na kuwaomba Wananchi kutoa ushirikiano kwa timu za wachanjaji watakapofika katika maeneo yao na kupita kwenye nyumba ili kutoa matone ya chanjo ya Polio kwa watoto walio chini ya miaka mitano.

Comments are closed