Tanzania kuwa mwenyeji maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.

Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC-AU) yatakayofanyika kesho Mei 25, 2024 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) amesema uenyeji huu umekuja kufuatia maamuzi ya Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2024 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

“Ikumbukwe kuwa, mwezi Machi 2022 Tanzania ilichaguliwa kuhudumu kwenye nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa miaka miwili hadi mwezi Machi 2024 ambapo muda wa kuhudumu ulifikia kikomo. Hivyo Tanzania imechaguliwa tena kuhudumu kwenye Baraza hilo kwa muhula mwingine wa miaka miwili hadi mwaka 2026,” alisema Waziri.

Amesema Baraza la Amani na Usalama ni chombo cha juu cha maamuzi kuhusu masuala ya amani na usalama kwenye Umoja wa Afrika likiwa na jukumu la kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza.

Nchi 15 tu kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika ndio wajumbe wa Baraza hilo na wajumbe wa sasa ni pamoja na; Tanzania, Uganda na Djibout (Ukanda wa Afrika Mashariki); Cameroon, DRC na Equatorial Guinea (Kanda ya Kati); Afrika Kusini, Angola na Botswana (Kanda ya Kusini); Cote d’Ivoire , Gambia, Nigeria, na Sierra Leone (magharibi) na Misri na Morocco (Ukanda wa Kaskazini).

‘’Hivyo, Tanzania kuwa Mjumbe kwenye Baraza hili ni ishara ya kuheshimika na kuaminika kwa nchi yetu, ambapo heshima hiyo inaifanya nchi yetu kupewa jukumu jingine kubwa zaidi la kuwa mwenyekiti wa Baraza hilo kwa mwezi Mei. Katika nafasi ya Uenyekiti Tanzania inajukumu la kusimamia shughuli zote zinazohusu Baraza, ikiwemo kufuatilia kwa karibu hali ya ulinzi na usalama kwenye Bara la Afrika, kutoa miongozo ya kushughulikia na masuala ya kiusalama pale inapobidi na pia kuandaa ratiba na kuongoza vikao vya Baraza,’’ alisema Waziri Makamba.

Katika maadhimisho hayo Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Baraza imeandaa ratiba ya shughuli mbalimbali kwa kuifanya kila wiki katika mwezi Mei kubeba dhima mahsusi ambazo ni: Usuluhishi na majadiliano; masuala ya mahitaji ya kibinadamu,amani na usalama; ulinzi kwa Watoto na kusaidia misheni za amani.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya Miaka 20 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika ni; ‘’Miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwa chombo cha Maamuzi: Miongo miwili ya Afrika ya Amani na Usalama tunayoitaka (20 years of the AU PSC as a Standing Decision-Making Organ: The Next Decades of the Peace and Security We Want in Africa)’’

Maadhimisho haya, yanatoa fursa kwa Waafrika wote wenye kuitakia mema Afrika kutoa maoni yao ya kuliimarisha Baraza ili liweze kushughulikia changamoto za kiusalama barani Afrika. Hivyo, wageni takriban 120 kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria.

Kadhalika, Miongoni mwa watu mashuhuri watakaoshiriki ni pamoja na; Jesca Alupo, Makamu wa Rais Uganda, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais Mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Burundi,. Domitien Ndayizeye, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano na Rais Mstaafu, wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.

Maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza yatahitimishwa kwa kutolewa kwa Tamko la Dar es Salaam.