Tanzania na Kenya zilivyozima maandamano ya maadhimisho ya Saba Saba

Tanzania na Kenya zimeimarisha ulinzi kwa kupeleka idadi kubwa ya maafisa wa polisi siku ya jana  ili kuzuia maandamano, huku mataifa hayo ya Afrika Mashariki yakichukua msimamo mkali zaidi dhidi ya maandamano ya wananchi.

 Nchini Tanzania, makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja na vyama vya upinzani yanadai kuwa maelfu ya watu waliuawa na vikosi vya usalama wakati wa vurugu zilizohusiana na uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, kufuatia madai ya wizi wa kura na mashambulizi dhidi ya wakosoaji wa serikali.

Nchini Kenya, angalau watu 127 waliuawa wakati wa maandamano yaliyotokana na ugumu wa maisha, ufisadi na ukatili wa polisi kati ya Juni na Julai mwaka 2024, pamoja na kipindi kama hicho mwaka 2025, kulingana na mamlaka inayosimamia utendaji wa polisi.

Wanaharakati walikuwa wameitisha maandamano ya amani tarehe 7 Julai, maarufu kama Saba Saba, siku inayokumbuka maandamano ya kihistoria katika nchi zote mbili.

Hata hivyo, uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama umezuia maandamano hayo kufanyika. Tanzania hivi karibuni ilipiga marufuku mikusanyiko yote ya kisiasa, huku polisi wa Kenya wakikataa kupokea taarifa za maandamano kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu.

Wakati huohuo, wananchi wengi wanaendelea kuogopa kutoa sauti zao hadharani.

“Siko tayari kuhatarisha maisha yangu,” alisema Hussein Matimbwa, mwenye umri wa miaka 33, mkazi wa Dar es Salaam, akizungumza na 

“Vifo vilivyotokea Oktoba mwaka jana vinatisha. Kuandamana ni haki ya kisheria, lakini hapa Tanzania unaweza kupoteza maisha kwa kushiriki tu kwenye maandamano,” aliongeza.

Polisi na wanajeshi walionekana wakisambazwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, huku eneo la biashara la Kariakoo likiwa tulivu isivyo kawaida na maduka mengi yakiwa yamefungwa.

Mkazi mmoja alisema alikuwa ametamani kushiriki maandamano lakini alikosa watu wa kumuunga mkono.

“Watu wengi wanaogopa kufa. Polisi na wanajeshi wako kila mahali wakiwa na bunduki,” alisema.

-Timu za siri za polisi-

Katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, polisi walifunga baadhi ya barabara na kuwatawanya waandamanaji wachache waliokuwa wamekusanyika katikati ya jiji.

Waandishi walishuhudia angalau watu watatu wakikamatwa na kupakiwa kwenye gari lisilo na alama za utambulisho pamoja na gari la polisi. Msemaji wa polisi alisema huenda ulikuwa “ukamataji uliofanywa na timu zetu za siri.”

“Kwa nini waweke ulinzi mkubwa kiasi hiki? Tuna haki ya kuandamana,” alisema mmoja wa waandamanaji hao, Collins Otieno.

Baadaye, Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Nairobi, Issa Mohamud, alisema watu 10 walikamatwa na watashtakiwa kwa kosa la kuzuia shughuli pamoja na makosa mengine yanayohusiana.

“Hatuna taarifa za vifo wala majeruhi, lakini tumefanya ukamataji,” aliwaambia waandishi wa habari.

Kundi la Economic Justice Movement lilikuwa limetangaza maandamano ya Jumanne kwa lengo la kuangazia mauaji yanayodaiwa kufanywa nje ya utaratibu wa sheria, watu kutoweka kwa lazima, ukamataji wa kiholela, ukatili wa polisi, pamoja na kuongezeka kwa matatizo ya uchumi na kupungua kwa fursa kwa mamilioni ya vijana na familia.

Hata hivyo, wengi wanaogopa kushiriki.

“Kuna hali ya uchovu na kukata tamaa miongoni mwa wananchi,” alisema Wanjira Wanjiru wa Mathare Social Justice Centre.

Rais wa Kenya, William Ruto, ameonekana kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya wakosoaji wake. Hivi karibuni aliikosoa kupitia mtandao wa kijamii gazeti la The Standard kutokana na taarifa zake ambazo zimekuwa zikimkosoa.