Rais Samia Suluhu Hassan leo amepokea ripoti ya Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa inayoongozwa na Prof Mukandala jijini Dar es Salaam
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Prof Mukandala amesema kuwa kwa mujibu wa maoni yaliyowasilishwa kwenye kikosi kazi, na wadau waliofika kutoa maoni, Watanzania wanaonekana wamegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza linaamini kwamba hakuna sababu ya kuwa na katiba mpya, na wanasema kwamba katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho, ili kuingiza matakwa ya wakati uliopo. Kundi la pili ni la wananchi wanaoamini kuwa ni muhimu kuwa na katiba mpya
Kikosi kazi kimewatenga wadau katika makundi matano.
- Wanaotaka Tanzania ianze upya mchakato wa kupata Katiba Mpya. Kikosi kazi kimeona hii itachukua muda na fedha nyingi.
- Wanaotaka mchakato uendelee ulipoishia. Kikosi kazi kimeainisha kuwa mchakato umepitwa na wakati.
- Wanaotaka Rasimu ya Pili ya Katiba (ya Tume iliyoongozwa na Jaji Warioba) ipigiwe kura. Kikosi kazi kimeona hatua hii haitekelezeki maana inabidi rasimu ipitishwe na Bunge.
- Wanaotaka tume maalum ya wataalam iundwe. Kikosi Kazi kimeona hii ndiyo ina mashiko.
- Wanaoona hakuna haja ya kuwa na Katiba Mpya
Katika kuwasilisha ripoti ya Kikosi Kazi hiyo, Mwenyekiti wao Prof Mukandala ameeleza hatua wanazozipendekeza zichukuliwe ili kupata Katiba Mpya. Hatua hizi kwa kifupi ni kama zifuatazo:
- Kuwepo na mjadala wa kitaifa ili kupata muafaka kuhusu muundo wa Muungano, madaraka ya Rais, uchaguzi, rushwa na mengineyo.
- Kuhuisha sheria ya Katiba na kura ya maoni na kuweka sharti la muda wa mchakato wa kutambua kuanzishwa kwa jopo la wataalamu watakaotengeneza rasimu ya Katiba Mpya.
- Kuundwa kwa jopo la watalaamu wa katiba watakaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.
- Rasimu hiyo ya jopo la wataalam ipelekwe bungeni ili ipitishwe kuwa Katiba Mpya.
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan amekipongeza Kikosi Kazi kwa kazi nzuri na amesema kuwa suala la Katiba ni suala zito sana na liko katika upande wa pekee na bado liko akilini hata hivyo ni vyema kushughulika na yale mepesi zaidi yaliyopo katika mapendekezo ya Kikosi kazi kuhusu mikutano ya vyama vya siasa, usawa wa kijinsia katika vyama na Bungeni na mengineyo.
“Kwa kifupi ni kwamba tumeyapokea na tutayafanyia kazi. Lakini ni muhimu wananchi wakaelewa kwamba maoni ya kikosi kazi sio amri kwa serikali kwamba ni lazima tukafanya kama ambavyo kikosi kazi kimesema.” amesema Rais Samia