Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa watu waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea mkoani Simiyu leo asubuhi, ikihusisha gari ya abiria na gari la waandishi wa habari. Kati ya watu waliofariki dunia, sita ni waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali huku wengine wakipata majeraha.
Watu hao wamefariki dunia baada ya gari la waandishi wa habari iliyokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel kugongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace katika eneo la Nyamikoma, Wilaya ya Busega katika Mkoa wa Simiyu.
Rais Samia amesema ameshtushwa na kutokea kwa ajali hiyo ambayo imegharimu maisha ya watu muhimu kwenye jamii huku akiwataka Watanzania kuwaombea majeruhi wapone haraka.
Katika ajali hiyo watu 11 walipoteza maisha papo hapo huku wengine 3 wakipoteza maisha muda mfupi baada ya ajali hiyo kutokea.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa waandishi wa habari waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Husna Mlanzi kutoka kituo cha televisheni cha ITV, Vanny Charles (Icon), Antony Chuwa, Johari Shani (Uhuru Digital) na Abel Ngapemba ambaye ni Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Waandishi hao wamefariki wakiwa wanaelekea katika majukumu yao ya kazi ambapo walikuwa katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gabriel kuelekea Wilaya ya Ukerewe kupitia Bunda.