Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Tanzania yaanza kuwahamisha Wamasai kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro - Mwanzo TV

Tanzania yaanza kuwahamisha Wamasai kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro

Tanzania ilianza kuwahamisha wafugaji wa Kimasai kutoka eneo maarufu la uhifadhi la Ngorongoro katika hatua ambayo wanaharakati wa haki walitaja kuwa kinyume cha sheria.

Jamii ya wamasai imeishi katika hifadhi hiyo, eneo la Urithi wa Dunia wa UNESCO kaskazini mwa Tanzania, kwa zaidi ya karne moja.

Lakini sasa wanakabiliwa na uhamisho, kwani mamlaka inadai kwamba idadi yao inayoongezeka ni tishio kwa makazi ya wanyamapori.

Maafisa wanasisitiza kuwa uhamisho huo ni wa hiari.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alisema karibu familia 296 zimejiandikisha kuhamia Handeni, wilaya iliyo umbali wa kilomita 600 kusini mwa Ngorongoro.

“Hakuna mtu nyeyote anaefurushwa, watu wote wanaondoka kwa hiari na serikali inawawezesha,” alisema katika taarifa yake ya video.

Serikali imetenga eneo la hekta 162,000 kwa kaya zilizohamishwa za Wamasai, alisema.

“Ufurushaji huu haujawahi kuwa wa hiari kwa watu wa Ngorongoro,” wakili wa haki za binadamu wa Ngorongoro na mwanaharakati Joseph Oleshangay aliiambia AFP.

“Nimeona maji, shule na hata umeme kwenye makazi mapya, kwa nini nisiende huko?” Alisema Edward Sapuru, mchungaji.

Uhamisho huo umezua wasiwasi, huku timu ya wataalam huru wa haki walioteuliwa na Umoja wa Mataifa wakionya kwamba unaweza kuhatarisha maisha ya Wamasai kimwili na kiutamaduni.

“Hii itasababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa, na inaweza kuwa kunyang’anywa mali, kufukuzwa kwa lazima na uhamishaji holela uliopigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa,” walisema katika taarifa Jumatano.

Tanzania kihistoria imeruhusu jamii za kiasili kama vile Wamasai kuishi ndani ya baadhi ya hifadhi za taifa.

Lakini tangu mwaka 1959, idadi ya watu wanaoishi Ngorongoro imeongezeka kutoka 8,000 hadi zaidi ya 100,000.

Idadi ya mifugo imeongezeka kwa haraka zaidi, kutoka karibu mifugo 260,000 mwaka 2017 hadi zaidi ya milioni moja leo.

Wamasai wanasema mamlaka inajaribu kuwalazimisha kuondoka katika ardhi yao ili kuandaa mazingira ya uwindaji wa kibinafsi kwa watalii.

Serikali imekataa tuhuma hizo, lakini suala hilo limesababisha mapigano kati ya wafugaji na polisi.

Askari mmoja aliuawa na waandamanaji kadhaa kujeruhiwa wakati wa maandamano wilayani Ngorongoro katika mji wa Loliondo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Maandamano hayo yalizuka kutokana na msukumo wa serikali wa kuziba eneo la kilomita za mraba 1,500 za Loliondo ili kujenga eneo la ulinzi wa wanyamapori.