Serikali ya Tanzania imebariki hoja yake ya kuwatambua na kuwasamehe walipakodi mahiri, huku mbunge mwenye hoja kinzani akiendeleza msisitizo wake kwamba anaona ishara ya kasoro na kashfa.
Akizungumza bungeni jijini hapa jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema serikali imezingatia dalili zote za walakini kabla ya kuupa baraka msimamo wake huo.
Kwa mujibu wa Dk. Nchemba jana kwenye mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka huu, miongoni mwa yaliyozingatiwa yanajumuisha mapitio ya vyombo vya ulinzi na usalama, kisha kubarikiwa na kikao cha Baraza la Mawaziri.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, aliyeasisi mada hiyo katika kikao cha Bunge awali, alitoa angalizo kwamba baraka hiyo ya msamaha inaweza kukaribisha hatari ya Rais kushauriwa vibaya, pia kufungua milango kwa kashfa za rushwa na ufisadi.
Mpina aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alisisitiza kwamba hatua hiyo ya Waziri wa Fedha na Mipango kupewa mamlaka ya kuwatambua walipakodi mahiri na kuwasamehe, ina hatari ya kuua morali kwa wawekezaji wa ndani, watakaonekana siyo mahiri kwa mtazamo wa waziri.
Alitaja maeneo ya hatari hizo, ni pale Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa msamaha huo, anaweza kushauriwa vibaya na baadhi ya watendaji na ikaleta shida kwa nchi.
“Ikiachwa hivyo serikali itakumbwa na kashfa, tutaweka wapi sura zetu na kwa nini tumweke?
“Kwa nini kuwa na misamaha ya kundi na mtu mmoja mmoja na kusema watu mahiri? Hii itaondoa ushindani. Kuna watu watasamehewa na wengine hawatasamehewa na wanaenda kushindana sekta moja,” alisema Mpina
Alifafanua ishara iliyo mbele ya hatari hiyo ni kufungwa viwanda huku vingine vikiendelea, msingi wa tatizo ukianzia katika tafsiri za misamaha hiyo ya kodi.
“Mimi napendekeza kama ni miradi ya kimkakati inahitaji msamaha, tuitungie sheria iletwe bungeni kwa utaratibu. Tukiacha hivi, watu watatumia nafasi hii kufanya ufisadi na tutaua uwekezaji nchini,” aliwasilisha.