Kampuni kubwa ya usafirishaji ya Dubai DP World ilitia saini mikataba mitatu siku ya Jumapili na serikali ya Tanzania ya kuendesha sehemu ya bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 30 chini ya mkataba wenye utata unaohusu bandari zote za nchi.
Mikataba hiyo mipya inaipa DP World usimamizi wa kipekee wa gati nne kati ya 12 za jiji na nyingine nne kwa ushirikiano na Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mikataba hiyo itapitiwa kila baada ya miaka mitano, alisema mkurugenzi mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.
Utiaji saini huo unafuatia makubaliano ya kiserikali yaliyotiwa wino Oktoba mwaka jana na Rais Samia Suluhu Hassan akifungua njia kwa DP World kusimamia bandari zote nchini Tanzania kwa kushauriana na serikali.
Ilivyoidhinishwa na bunge na kuzua maandamano
Mnamo Juni 10,2023 bunge la Tanzania liliridhia Azimio la serikali kuhusu Mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii wa Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari Tanzania.
Azimio hilo liliwasilishwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitza kuwa pamoja na Serikali kuchukua hatua mbalimbali za maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, bado ufanisi katika utoaji huduma za bandari haujafikia viwango vinavyotakiwa kimataifa.
“Hali ya sasa ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda”
Wakosoaji wa mpango huo wanasema ni tishio kwa mamlaka na usalama wa Tanzania, lakini serikali imesema kuwa itaboresha ufanisi, kupunguza gharama na kuongeza mapato.
Mkurugenzi Mtendaji wa DP World Sultan Ahmed bin Sulayem alisema hatua hiyo itaruhusu kampuni hiyo “kuboresha bandari ya Dar es Salaam kuwa kituo cha hadhi ya kimataifa, na kujenga kituo kikubwa zaidi cha usafirishaji kwa Tanzania.”
Kampuni inayodhibitiwa na serikali ya Dubai imeahidi kuwekeza dola milioni 250 katika kipindi cha miaka mitano ijayo katika bandari hiyo, mojawapo kubwa zaidi katika bara la Afrika.
Takriban watu 22 wamekamatwa tangu Juni kwa kupinga mpango huo, kulingana na Amnesty International, ingawa baadhi yao wameachiliwa.
Wakili Rugemeleza Nshala ni miongoni mwa walioachiliwa na kusema alilazimika kuondoka nchini mwezi Julai baada ya kupewa onyo na vitisho vya kuuawa.
Rais Samia anena, asema milango ipo wazi sekta binafsi kuwekeza
Akizungumza mara baada ya mikataba hiyo kusainiwa Rais wa Samia amesema maendeleo ya nchi ni shirikishi, hivyo milango ipo wazi kwa sekta binafsi kuwekeza nchini na kufanya biashara.
“Kila pale ambapo sekta binafsi inaweza kuweka fedha na sisi serikali fedha ile tusiiweke tukaitumia kwenye mambo mengine ya maendeleo,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo,Rais amewatoa hofu Watanzania kwa kusema hakuna atakayepoteza ajira kutokana na uwekezaji huu wa DP World.
“Kama alivyosema Mkurugenzi (Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Plasduce Mbossa) hakuna atakayepoteza kazi ima muajiriwa wa bandari hata wanaofanya kazi bandarini,” amesema Rais Samia na kuongeza
“Tumezingatia maoni ya makundi mbalimbali kabla ya kusaini mkataba huu” alisema Rais Samia.
Aidha amesema mikataba iliyoingiwa kati Serikali na kampuni ya DP World ya nchini Dubai, inaenda kuongeza mapato ya serikali, hivyo kukuza uchumi wa taifa.
Amesema bandari ya Dar es Salaam ni lango la biashara kwa nchi zinazozunguka, hivyo ni wajibu kuwekeza, kuboresha na kuhudumia nchi zinazoizungukaTanzania kama nyenzo ya kiuchumi pia kwa kuzingatia mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN), unazozitaka nchi za mlango bahari kuhudumia nchi nyingine.
Aliingia madarakani Machi 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake John Magufuli akiahidi uhuru zaidi wa kisiasa.
– ‘Weka mkataba hadharani’ –
Lakini wakosoaji walimtaja kuwa “dikteta” baada ya Freeman Mbowe, kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema, kukamatwa kwa tuhuma za ugaidi Julai 2021 kabla ya kuachiliwa.
Chadema ilikuwa miongoni mwa waliopinga mpango huo unaoipa DP World haki ya kipekee kwa muda wa miezi 12 kujadiliana na serikali kuhusu namna bora ya kusimamia bandari 80 za nchi.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe na Mkuu wa Kanisa Katoliki Tanzania Charles Kitima pia walijitokeza kupinga mpango huo lakini walihudhuria utiaji saini wa Jumapili.
“Baadhi ya mapendekezo yetu yamezingatiwa,” ilisema taarifa ya ACT-Wazalendo. “Lakini bado tunasisitiza kwamba mkataba huo uwekwe hadharani.”