Seikali ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kulinda na kuendeleza haki za binadamu, utawala bora na utawala wa sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Dkt. Abdallah S. Possi, wakati wa majadiliano ya wazi kuhusu taarifa ya mwaka ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Tanzania, Dkt. Possi alieleza kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi, na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa vya haki za binadamu.
“Tanzania inaendelea kulinda uhuru wa kujieleza, haki ya kupata taarifa, na ushiriki wa vyombo vya habari. Tunaamini katika usawa mbele ya sheria kwa watu wote, wakiwemo watetezi wa haki za binadamu,” alisema Dkt. Possi.
Katika hotuba yake, Dkt. Possi alijibu wasiwasi ulioelezwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu madai ya utekaji, kukandamizwa kwa uhuru wa kisiasa na nafasi ya kiraia, mateso, na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Alibainisha kuwa serikali ya Tanzania inachukulia kwa uzito madai hayo, na imekuwa ikifanya uchunguzi wa kina kuhusu kila tukio linaloripotiwa.
Aidha, alieleza kuwa hakuna msamaha kwa wale wanaobainika kuvunja sheria za haki za binadamu.
“Sheria ya nchi inalinda haki ya kuishi, uhuru na usalama wa mtu. Taarifa za utekaji au kutoweka kwa watu zinachunguzwa kwa kina, na serikali inatekeleza wajibu wake wa kikatiba katika kushughulikia matukio haya,” alisisitiza.
-Uchaguzi Huru na wa Haki Watajwa-
Kwa mujibu wa Dkt. Possi, kupitishwa kwa Sheria ya Uchaguzi ya Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 ni hatua muhimu katika kuhakikisha mazingira bora ya uchaguzi.
Sheria hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali na inalenga kuweka uwanja sawa kwa vyama vyote vya siasa.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefungua milango kwa mashirika ya ndani na nje kutuma maombi ya kutoa elimu ya uraia na kushiriki kama waangalizi wa uchaguzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uwazi na ushirikishwaji.
-Sakata la wageni wa kisiasa lafafanuliwa-
Kuhusu tukio la hivi karibuni linalowahusisha watetezi wa haki za binadamu kutoka nje ya nchi, Boniface Mwangi kutoka Kenya na Agatha Atuhaire kutoka Uganda, alieleza kuwa Wanaharakati hao walirudishwa kwao baada ya kukiuka sheria za uhamiaji.
Balozi Possi alisisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria, wageni wote wanatakiwa kutoa sababu halali na za kweli za kuingia nchini.
“Kuwa mtetezi wa haki za binadamu hakumfanyi mtu kuwa juu ya sheria za nchi nyingine. Heshima kwa sheria ni msingi wa ushirikiano wa kimataifa,” aliongeza.
Tanzania imetumia jukwaa hilo la kimataifa kuonesha kwamba inathamini mazungumzo ya kimataifa kuhusu haki za binadamu na iko tayari kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa 2025 unakuwa wa kidemokrasia na wa kuigwa.
“Serikali ya Tanzania inabaki na dhamira ya dhati ya kulinda haki za binadamu, kudumisha amani, na kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa kupitia mchakato wa kidemokrasia,” alisema Balozi Possi akihitimisha hotuba yake.