Tanzania yajitetea UNHRC, yakemea mataifa ya Magharibi kwa tathmini yenye upendeleo

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha msimamo wake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), ikikosoa baadhi ya nchi za Magharibi na taasisi za kimataifa kwa kile ilichodai kuwa ni mtazamo wa upande mmoja kuhusu hali ya usalama nchini baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Katika taarifa ya haki ya kujibu iliyotolewa Machi 2, 2026 mjini Geneva, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa, Balozi Ally Possi, alisema serikali imelazimika kutoa ufafanuzi kufuatia kauli za wawakilishi wa Ubelgiji, Uingereza, Uswisi, Sweden, Ireland, Norway, Jumuiya ya Ulaya (EU), pamoja na mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International.

Tanzania ilikanusha kwa nguvu zote tuhuma za mauaji ya kiholela, hasa zile zilizotolewa na Uingereza, ikisema baadhi ya washirika wa kimataifa wamepuuza mazingira halisi yaliyopelekea matukio ya vurugu. 

Kwa mujibu wa serikali, Oktoba 29, 2025 kuliripotiwa mashambulizi iliyoeleza kuwa yalilenga vituo vya polisi, majengo ya serikali na miundombinu muhimu ya umma.

Katika tamko hilo, Balozi Possi alieleza  kuwa matukio hayo hayakuwa ya bahati mbaya, bali yalidaiwa kupangwa kwa makusudi kwa nia ya kuvuruga utaratibu wa kikatiba na kusababisha taharuki nchini. Iliongeza kuwa baadhi ya matamshi ya kimataifa yameacha kwa makusudi kuangazia chanzo cha mgogoro huo.

Alisisitiza  kuwa Serikali ina jukumu la kikatiba la kulinda amani na usalama wa wananchi wake, na kwamba hatua zilizochukuliwa na vyombo vya dola zilifuata misingi ya kisheria kwa lengo la kuzuia kuenea kwa machafuko.

Aidha, ilizitaka nchi washirika na jumuiya ya kimataifa kuheshimu mamlaka ya Tanzania kama taifa huru, na kuepuka kutoa hitimisho kabla ya taratibu za ndani kukamilika.

Kuhusiana na wito wa kuundwa kwa uchunguzi huru, serikali ilieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan tayari ameunda Tume Huru ya Uchunguzi kwa mujibu wa sheria za nchi. Tume hiyo inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake Aprili 3, 2026.

Kwa mujibu wa serikali, mapendekezo ya tume hiyo yatatumika kama mwongozo katika juhudi za kuimarisha maridhiano ya kitaifa, kusukuma mbele mageuzi ya kikatiba yanayopangwa, pamoja na kuboresha mifumo ya taasisi kwa lengo la kuendeleza demokrasia.

Katika kuhitimisha, Tanzania imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusubiri matokeo ya mchakato huo rasmi, ikisisitiza kuwa inaendelea kushikilia misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na mazungumzo ya kujenga kwa maslahi ya taifa.