Tanzania na Benki ya Dunia zimetiliana saini mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 650 sawa na shilingi trilioni 1.5 za kitanzania kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi (BOOST) na mradi wa kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi nchini.
Mikataba hiyo imesainiwa na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi. Mara Warwick.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Bw. Tutuba alisema kuwa fedha hizo zimetolewa na Benki ya Dunia kupitia mgao wa masharti nafuu wa Mzunguko wa IDA 19, ambapo dola za Marekani milioni 500 zitatumika kuboresha elimu ya msingi na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 150 kitatumika kuimarisha usalama wa milki za ardhi hapa nchini.
Bw. Tutuba alisema kuwa miradi iliyo chini ya Mikataba iliyosainiwa inatekeleza Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26), na ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inayolenga kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu kupitia mikakati mbalimbali.
Alifafanua kuwa katika sekta ya elimu ya msingi, fedha hizo zitatumika kuboresha na kusimamia mazingira shirikishi ya kufundishia na kujifunzia, kuboresha uwezo wa walimu, kukuza na kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika shule za awali na msingi.
Mradi wa BOOST unakusudia kuboresha usawa katika upatikanaji wa elimu bora ya awali na msingi kwa upande wa Tanzania Bara ukiwemo ujenzi wa vyumba 12,000 vya madarasa pamoja na vifaa vinavyohitajika vya elimu; usimikaji wa mifumo na usambazaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule na vyuo vya ualimu 800 kwa pamoja; na kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za awali na msingi.
Bw. Tutuba alisema kuwa katika sekta ya ardhi, kazi zitakazofanyika ni kukuza na kuwezesha upangaji, upimaji na utoaji hatimiliki za ardhi kwa ajili ya uwekezaji na usalama wa makazi ya watu, kuboresha na kuongeza mfumo unganishi wa taarifa za usimamizi wa ardhi na kukuza matumizi ya TEHAMA katika upimaji na uandaaji wa hatimiliki ya ardhi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia hapa nchini Bi. Mara Warwick alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha elimu na kwamba fedha zilizotolewa na Benki hiyo kama mkopo nafuu zitawanufaisha zaidi ya wanafunzi 12,000 wanaosoma masomo ya awali na elimu ya msingi.