Tanzania yapewa msaada wa bilioni 210 kutoka Ujerumani

Ujerumani imepatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni 210 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya sekta za afya, maji, utalii, mazingira, utawala bora, kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuboresha mfumo wa kidijitali kwa ajili ya kufuatilia matukio ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

Ujerumani imetangaza uamuzi huo mjini Berlin baada ya kukamilika kwa majadiliano kati ya ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Ujumbe wa Ujerumani ulioongozwa na Naibu Waziri anayesimamia uhusiano wa kiuchumi na Maendeleo wa nchi hiyo, Dkt. Barbel Kofler.

“Serikali ya Tanzania inafuraha kupokea msaada wa Euro milioni 87 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 210, utakaosaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha Maisha ya watu” alisema Dkt. Nchemba wakati akitoa neno la shukrani baada ya kusainiwa kwa nyaraka za makubaliano ya msaada huo.

Dkt. Nchemba alifafanua kuwa msaada huo utaelekezwa kutunza baioanuai ya Hifadhi za Taifa na maeneo ya uwindaji ili kutunza mazingira ya maeneo hayo kwa kuongeza mapato na kuwa na utalii endelevu.

“Msaada huo pia unakusudia kuboresha afya ya mama na mtoto, kuimarisha uzazi wa mpango hususan kwa vijana na mpango wa bima ya afya kwa wote” alieleza Dkt. Nchemba

Alisema kuwa eneo lingine ambalo fedha hizo zitaelekezwa ni pamoja na usafi wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji ili kuwawezesha watu wengi kupata maji safi na salama ya kunywa Tanzania Bara na Visiwani.

Dkt. Nchemba alisema kuwa sehemu ya msaada huo pia itaelekezwa kwenye jamii ikiwemo usawa wa kijinsia, kuimarisha haki za wanawake na Watoto kwa kuzuia kila aina ya vitendo vya ukatili dhidi yao ili kuharakisha maendeleo ya nchi

Alisema kuwa usimamizi na utawala bora wa fedha za umma, na kuboresha mifumo ya fedha ni miongoni mwa faida zitakazotokana na msaada huo pamoja na sehemu ya fedha hizo kutumika katika masuala ya utafiti na uandishi wa miradi inayokusudiwa kutekelezwa na serikali kupitia mfuko wa mafunzo na utaalam.

Dkt. Nchemba alifafanua Zaidi kuhusu miradi itakayonufaika na fedha hizo kuwa ni mradi wa Hifadhi ya mfumo wa ikolojia wa Serengeti, Mradi wa Hifadhi ya ikolojia ya Selous na Nyerere,  mradi wa kuboresha afya Tanzania awamu ya pili, kuimarisha haki za wanawake na Watoto, kujenga kituo cha mfumo wa kidijitali kwa ajili ya taarifa za haki za raia na usawa wa kijinsia, mradi wa usalama wa maji maeneo ya mijini Tanzania Bara na Zanzibar,  kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na masuala ya utafiti na utaalam. 

“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ninaishukuru Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kwa msaada huu mkubwa na nikuhakikishie kuwa tutafuatilia matumizi ya fedha hizi kwa karibu zaidi ili manufaa yaliyokusudiwa yapatikane” alisisitiza Dkt. Nchemba.