Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza Serikali kwa kufanikiwa kupunguza vifo vya akinamama wajawazito kutoka vifo 556 556 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 104 mwaka 2022.
Dkt. Kikwete amesema hayo leo wakati akifungua kongamano la pili la kisayansi la afya ya uzazi mama na mtoto ambalo linafanyika jijini Dar Es Salaam linalojumuisha wataalam mbalimbali wa sekta ya afya.
Dkt. amesema mwaka 2000 hadi 2015 katika malengo ya Milenia yalitaka nchi zinazoendelea kupunguza vifo vya akinamama wajawazito kufikia 191 kwa kila vizazi hai laki moja, lakini Tanzania mwaka 2015 tulifikia vifo 432 katika vizazi hai laki moja na vikaendelea kuongezeka hadi kufikia 556 mwaka 2016.
“Mwelekeo wa sasa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni mzuri, vifo vimepungua kutoka 556 mwaka 2016 hadi kufikia 104. Hii ni hatua kubwa naipongeza Serikali na Wizara ya Afya kwa jitihada ilizoweka. Ni jambo la kufedhehesha kuona mama ambaye analeta uhai wa kiumbe duniani anapoteza maisha”. AmesemaKikwete.
Kwa upande wake Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amemshukuru Dkt. Kikwete katika awamu yake ya uongozi kwa kutambua na kuthamini huduma za afya ya uzazi ambapo mwaka 2014 alizindua mpango wa kuchochea huduma bora za afya ya uzazi ili kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na Watoto.
Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kuboresha huduma bora za afya kwa Watanzania katika ujenzi wa miundombinu ya afya katika maeneo mengi, upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba, kuajiri watumishi wa afya pamoja na kujengea uwezo watumishi wa afya.
Hata hivyo, akitolea mfano wa kifo cha mama mjamzito kilichotokea hivi karibuni Mkoani Tanga, Waziri Ummy ametoa wito kwa watumishi wa afya watakaoshindwa kutimiza majukumu yao kazini kuwa hatasita kuchukua hatua za kuwafutia usajili madaktari na manesi watakaobainika kuhusika na kifo hicho huku akiongeza kuwa hatua ziluzochukuliwa hivi sasa ni za kiutawala ambazo wanaotuhumiwa wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Waziri Ummy amesema kama kutakua na tuhuma za jinai kwa wataalam hao watapelekwa mahakamani, hivyo amewataka wananchi kuwa na uvumilivu katika kipindi ambacho kamati inaendelea na uchunguzi na endapo ukikamilika majibu yake yatawekwa wazi ili kila mwananchi ajue kilichotokea.