Search
Close this search box.
Africa

Serikali ya Tanzania imepokea shehena ya chanjo aina ya Sinopharm dozi 3,000,000 zitakazowakinga Watanzania 1,500,000 dhidi ya Uviko-19 zilizotolewa kwa hisani ya mke wa Rais wa China, Profesa Peng Liyuan.

Chanjo hizo zinapokelewa wakati mpaka kufikia Julai 12, 2022 Watanzania 10,511,804 walikuwa wamekamilisha dozi ya Uviko-19 huku Tanzania ikiwa imepokea jumla ya dozi 21,226,520.

Hayo yamesemwa leo Julai 14, 2022 na Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya, Dk Beatrice Mutayoba wakati akipokea chanjo hizo na kuongeza kuwa mpaka sasa jumla ya chanjo zilizotolewa na Serikali ya China zimefikia 6,000,000.

“Chanjo hizi zimethibitishwa na WHO, tunasisitiza Watanzania wachanje kwani ili kufikia kinga jamii lazima asilimia 70 ya walengwa ambao ni watu milioni 21,518,649 wawe wamechanja lakini mpaka sasa tumefikia watu milioni 10,511,804 ambao ni sawasawa na asilimia 32.91,” amesema Mutayoba.

Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Tanzania, Salem Chu Kun amesema chanjo hizo milioni tatu zilizotolewa na mke wa Rais wa China zimeelekezwa zaidi kwa kundi la wanawake.

“Awali Serikali ya China ilikuwa ikishirikiana na Tanzania, Profesa Peng ametoa chanjo hizi kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania lengo kuhakikisha wananchi wanapata chanjo ya Uviko-19,” amesema Chu Kun.

Mkurugenzi wa masuala ya wanawake kutoka wizara ya maendeleo ya jamii, wanawake, watoto na makundi maalum, Grace Mwangwa amesema jamii hususan wanawake na makundi maaalum.

“Tunawashkuru sana kwa kuipa nchi yetu kipaumbele, ni wajibu wetu kuona wanawake wanapewa umuhimu katika eneo hili, kwa kuwa katika janga hili wanaoathirika kwa kiasi kikubwa ni wanawake na wao ndiyo wanaotumika zaidi katika utunzaji wa familia na ndiyo wanaowajibika, uviko umeathiri hasa wanawake na makundi maalum,” amesema.

Comments are closed