Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendreleo ya Makazi imesaini Hati ya Makubaliano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN- HABITAT), kuanzisha ofisi nchini humo, kuboresha makazi holela sambamba na kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Makubaliano mengine ni kusaidia matumizi jadidifu ya nishati katika majengo, kupitia na kuandaa sera mpya ya miji, kuanzisha kituo cha taarifa ya makazi pamoja na kuboresha mifumo ya kitaasisi na uendelezaji miji midogo.
Makubaliano ya pande hizo mbili yamesainiwa jijini Nairobi nchini Kenya juzi mbele ya Mkutano wa Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT) na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Maimunah Mohd Sharif.
Aidha, makubaliano yaliyofikiwa yatawezesha pia Shirika la Makazi Duniani kuanzisha ofisi yake nchini Tanzania ili kurahisisha utekelezaji wa makubaliano hayo.
Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo, Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula amelihakikishia Shirika la UN-HABITAT kuwa Tanzania iko tayari kulipatia shirika hilo jengo la kuanzisha ofisi nchini.
Aidha, Dkt Mabula amelishukuru Shirika la UN-HABITAT kwa misaada mbalimbali inayoipatia Tanzania sambamba na kupongeza uamuzi wa shirika hilo kuanzisha ofisi nchini Tanzania.
‘’Naiomba UN-HABITAT kusaidia kuwajengea uwezo watanzania kwa kuwapa mafunzo na ajira za muda mfupi na mrefu ili kuwajengea uwezo’’ alisema Dkt Mabula
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UN-HABITAT Maimunah Sharif alisema, malengo endelevu ya Makazi na Nyumba yatafikiwa haraka kwa shirika lake kuwa na ofisi ya kudumu nchini Tanzania na nchi nyingine wanachama wa shirika hilo.
Alisema, Shirika lake kwa sasa linafanya maandalizi kabambe ya kuanzisha ofisi zake nchini Tanzania ili kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo pamoja na kuondoa makazi holela ili kuwa na miji salama na iliyopangwa.
‘’niihakikishie Tanzania kuwa, UN-HABITAT iko tayari kutoa mafunzo na ajira za muda ili kuwajengea uwezo watanzania na kusaidia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa’’ alisema Maimunah.
Kufunguliwa kwa ofisi za Shirika la Makazi Duniani la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kutaharakisha maendeleo endelevu ya sekta ya Makazi na Nyumba na kutatoa ajira kwa watanzania.
UN-HABITAT ni miongoni mwa mashirika ya umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi ya watu na Maendeleo endelevu ya Miji na lilianzishwa mwaka 1977 kama matokeo ya mkutano wa kwanza wa umoja wa mataifa wa Makazi ya watu na Maendeleo endelevu ya miji uliofanyika Vancouver , Canada mwaka 1976.
Katika hatua nyingine, Tanzania na Kenya zimejadili kuboresha mahusiano katika sekta ya nyumba na makazi ambapo kwa upande wakeWaziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema serikali ya Tanzania iko makini kusimamia maendeleo ya sekta nyumba na makazi ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu mijini linalofikia asilimia 4.8 kwa sasa.
‘’Moja ya juhudi za serikali ni utekelezaji wa mpango wa miaka 10 wa kurasimisha makazi holela ulioanza mwaka 2013’’ alisema Dkt Mabula
Kwa upande wake Waziri wa Kenya anayeshughulikia masuala ya Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Zacharia Mwangi Njeru amesema nchi yake imeanzisha mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu utakaowezesha ujenzi wa nyumba laki mbili kila mwaka.
Viongozi hao wawili walikubaliana kuunda kamati ya wataalamu wa pande zote mbili watakaosimamia utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo yaliyosainiwa mwaka 2021 jijini Dar es Salaam.