Tanzania yasaini mkopo wa shilingi bilioni 70 Abu Dhabi

Tanzania imetia saini mkopo wenye masharti nafuu wa shilngi bilioni 69.9 (dola milioni 30) na Mfuko wa Maendeleo wa Adu Dhabi kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Benaco hadi Kyaka mkoani Kagera. 

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesaini mkataba huo wa mkopo na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo Mohammed Saif Al Suwaidi ili kuwezesha ujenzi wa njia ya msongo wa kV 220 yenye urefu wa kilometa 167. 

Taarifa ya Wizara ya Fedha iliyotolewa leo Agosti 9, imesema mkopo huo pia utasiaida katika upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kyaka kilichopo Kagera. 

Tukio hilo limeshuhudiwa na Viongozi mbalimbali wa Tanzania na Mfuko huo, akiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania-Falme za Nchi za Kiarabu-Luteni Jenerali (Mstaafu) Yacoub Hassan Mohammed na  Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bw. Lawrence Mafuru.

Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Bw. Maharage Chande, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Bw. Rished Bade, Kamishna Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa, Bw. Japhet Justin, pamoja baadhi ya Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania UAE.