Tanzania yatuma risala za rambirambi kwa waathiriwa wa ajali ya ndege

Watanzania waliokuwa na majonzi Jumatatu walituma risla za rambi rambi kwa watu 19 waliofariki dunia wakati ndege ya abiria ilipotumbukia Ziwa Victoria katika ajali mbaya zaidi ya anga kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa nchini humo.

Ndege ya Precision Air kutoka mji mkuu wa kifedha wa Dar es Salaam ilianguka Jumapili asubuhi ilipokuwa ikijaribu kutua kaskazini magharibi mwa jiji la Bukoba.

Hali mbaya ya hewa ililaumiwa kwa ajali hiyo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa ni miongoni mwa mamia ya watu waliokusanyika kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, huku viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo wakiongoza maombi ya kuwaombea marehemu huku watazamaji wakifuta machozi.

Hafla ya kukabidhi miili ya wahanga kwa familia zao inatarajiwa kuchukua saa kadhaa, huku watangazaji wa eneo hilo wakirusha matangazo ya moja kwa moja kutoka uwanjani hapo.

Watu 24 walionusurika waliokolewa kati ya watu 43 waliokuwa kwenye ndege ya PW 494, huku wachunguzi kutoka Precision Air na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania wakiwasili katika jiji hilo la kando ya ziwa siku ya Jumapili.

Precision Air, kampuni iliyoorodheshwa hadharani na mchukuzi mkubwa wa kibinafsi nchini Tanzania, ilisema ndege hiyo ni ATR 42-500, iliyotengenezwa na kampuni ya ATR yenye makao yake makuu Toulouse, na ilikuwa na abiria 39 — akiwemo mtoto mchanga — na wafanyakazi wanne waliokuwa kwenye ndege hiyo.

Wafanyakazi wa dharura walijaribu kuinua ndege kutoka majini kwa kutumia kamba, wakisaidiwa na korongo huku wakazi pia wakitaka kusaidia.

Rais Samia Suluhu Hassan Jumatatu alitoa pole kwa familia za wahasiriwa, akiwapongeza wafanyikazi wa dharura na watu wa kujitolea kwa kuchukua hatua haraka kuokoa maisha.

“Nawapongeza walioshiriki uokoaji wakiwemo wananchi wa Bukoba,” alisema kwenye Twitter.

“Nawaombea marehemu wapumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka.”

Precision Air, ambayo kwa kiasi fulani inamilikiwa na Shirika la Ndege la Kenya Airways, ilianzishwa mwaka 1993 na inaendesha safari za ndege za ndani na nje ya nchi pamoja na kukodisha ndege za kibinafsi kwa maeneo maarufu ya kitalii kama vile Hifadhi ya Kitaifa ya Serengeti na visiwa vya Zanzibar.

Ajali hiyo inajiri miaka mitano baada ya watu 11 kufariki dunia wakati ndege ya kampuni ya safari ya Coastal Aviation ilipoanguka kaskazini mwa Tanzania.

Mwaka 1999, watu dazeni, wakiwemo watalii 10 wa Marekani, walifariki katika ajali ya ndege kaskazini mwa Tanzania wakati wakiruka kati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na uwanja wa ndege wa Kilimanjaro.