Tanzania yawasafirisha raia wake waishio nchini Sudan

Serikali ya Tanzania imesema imewasafirisha raia wake 200 kutoka Sudan kuja Tanzania ili kuwanusuru na mapigano makali yanayoendelea nchini humo.

Watanzania hao wamesafirishwa kwa njia ya basi kuelekea Ethiopia ambako watapanda ndege ya Air Tanzania kwa safari ya kurejea nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax ametoa taarifa hiyo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari akisema wamefanikiwa kuwasafirisha Watanzania 200 ambao ni wanafunzi na maofisa wa ubalozi.”

“Leo ndio wamefika mpakani na Ethiopia na wakifika huko watakuta ndege ya Air Tanzania inawasubiri kuwarudisha Tanzania,” amesema Dk Tax.

Amesema katika safari hiyo wamesaidia kuwabeba pia raia wa mataifa mengine ya Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia, Kenya na Msumbiji.Ameongeza kwamba Watanzania wengine pia walisaidiwa kusafirishwa na nchi nyingine za Uganda na Saudi Arabia. 

“Kazi hii siyo ndogo ndugu zangu, ni kazi ngumu kweli. Namshukuru Rais Samia kwa maelekezo yake, nawashukuru maofisa wa ubalozi kwa kusimamia safari hii.Muda wowote watawasili nchini tutawapokea,” amesema Waziri Tax.

Hadi sasa, zaidi ya watu 400 wameuawa kwenye mapigano hayo yanayohusisha vikosi vya jeshi la serikali na kikundi cha Rapid Support Forces (RSF). Wengiine zaidi ya 3,500 wamejeruhiwa