Tanzania yaweka mikakati kudhibiti homa ya Marburg

Siku mbili baada ya kutangazwa kuibuka kwa ugonjwa wa Marburg nchini Tanzania Serikali ya nchi hiyo imetoa mwongozo kwa wasafiri kote kwa kuzingatia kanuni za kimataifa, huku ikiagiza utekelezaji wake uanze mara moja.

Mwongozo huo namba 13 umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya nchi humo , Dk Seif Shekalaghe kwa kuzingatia kanuni za kimataifa za afya ya mwaka 2005 ili kutekeleza hatua madhubuti zinazohusiana na usafiri wa kimataifa.

Kwa mujibu wa mwongozo huo wasafiri wote wanaoondoka na wa ndani kutoka Mkoa wa Kagera watahitajika kujaza fomu ya mtandaoni ya ufuatiliaji wa wasafiri kupitia wavuti www.afyamsafiri.moh.go. .tz

Dk Shekhalaghe ameagiza kuwa watu wote walio katika orodha ya ufuatiliaji kutokana na kuwa karibu na wagonjwa wanapaswa kufuatiliwa mara kwa mara na kuzuiwa kuondoka katika maeneo yao ya kujitenga na kusafiri.

“Kwa wasafiri wote wanaoingia katika viwanja vya ndege, kivuko cha ardhini au bandari, watapimwa halijoto ya mwili na kwamba watu wote wataokutwa na hali ya homa wanapaswa kuzuiwa kusafiri ndani na nje ya nchi hadi watakapomaliza muda wa ufuatiliaji na kupewa kibali cha kusafiri na Mamlaka ya Afya ya Bandari,” amesema Dk Shekalaghe.

Aidha wasafiri wote watapewa kadi za maelezo ya afya zenye nambari ya bila malipo ambayo ni  199 na wanashauriwa kujifuatilia na kuripoti iwapo wana dalili za Marburg huku wale walio na alama na dalili watapimwa na kutibiwa katika vituo vya afya vya Serikali vilivyoteuliwa kuhudumia wagonjwa hao.

“Wakiwa nchini, wasafiri wote wa kimataifa wanapaswa kuzingatia kanuni za kuzuia na kudhibiti maambukizi kama vile usafi wa mikono, kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu na  kuripoti ishara au dalili zozote kwa kutumia nambari ya bure.

“Wamiliki wote wa vyombo vya usafiri wanapaswa kuzingatia kanuni zote za kinga na udhibiti wa maambukizi pamoja na usafi wa mikono na matumizi ya vipukusi,” amesema.

Dk Shekalaghe amesisitiza kuwa wasafiri wote wanapaswa kuzingatia hatua za kuingia, kutoka na kaguzi zote zinazotekelezwa ndani ya nchi.

Machi 21 Serikali kupitia Wizara ya Afya ilithibitisha uwepo wa ugonjwa Marburg katika Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangereko, Vijiji vya Bulinda na Butayaibega, ambao uliua watu watano na watatu kupata maambukizi huku watu 161 wamefuatiliwa na wanachunguzwa.

Shirika la Afya Duniani WHO linasema ugonjwa wa Virusi vya Marburg unaua kwa wastani nusu ya walioambukizwa. Virusi hupitishwa kutoka kwa popo wa matunda na huenea kati ya wanadamu kupitia majimaji ya mwili.

Ingawa hakuna chanjo au matibabu, wale wanaogunduliwa nayo hupewa maji kwa mdomo au kwa njia ya mishipa kwani madaktari hutibu dalili maalum za mgonjwa.