Wizara ya Afya nchini Tanzania imewaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha wanajiandaa ipasavyo ikiwa itatokea mgonjwa mwenye dalili za Ebola wapi atatengwa ili kutibiwa, timu ya wataalamu, ambulance na eneo la maziko iwapo kifo kitatokea.
Maagizo hayo yametolewa siku nane tangu kutokea mlipuko wa ugonjwa huo Septemba 20, 2022 katika Wilaya ya Mubende nchini Uganda ambapo mpaka sasa tayari vifo 23 vimetokea na wagonjwa 43.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 28, 2022 na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu wakati akitoa tamko la pili kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo nchini Uganda mbele ya vyombo vya habari.
“Kwa mamlaka niliyopewa nawaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kila mkoa kujiandaa na ni lazima waainishe ni gari lipi la wagonjwa ‘ambulance’ itatumika, timu ya wataalamu wa afua, mtu wa maabara ni yupi na mgonjwa akipatikana anapelekwa wapi, kuhakikisha kuna vifaa na atapelekwa wapi” amesema .
“Tusidharau tetesi yoyote kuhusu wahisiwa wa Ebola na kuandaa maeneo ya mazishi tukipata kifo cha mgonjwa wa ebola leo tunapaswa kwenda kumhifadhi wapi, wakuu wa mikoa kufuatilia maelekezo kwani wagonjwa wanatakiwa kutengwa,” amesema Waziri Ummy.
Pia ametoa maelekezo kwa jamii kusitisha safari zote hasa kuepuka kutembelea maeneo hatarishi yenye ugonjwa, kula nyama ambayo haijapikwa vizuri, kuepuka kugusa mate, machozi na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni.
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Dk Beatrice Mutayoba ameitaka jamii kujenga tabia ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na kufufua miundombinu ya kunawa sehemu zote zenye mikusanyiko.
“Tunasisitiza ushirikishwaji wa jamii tetesi za aina yoyote kwa urahisi kabisa na bila gharama mwananchi yeyote anaweza kupiga simu na kutoa taarifa dalili za Ebola na magonjwa mengine ili kuchukua tahadhari mapema kwa jamii lakini pia kwa wahudumu wa afya madhara ya ugonjwa ni makubwa na uwezekano wa kusababisha vifo ni mkubwa,” amesema.
Amesema timu ya wataalamu katika maeneo husika tayari imeweka ulinzi kwenye mipaka isiyohalali kwa ulinzi shirikishi na ulinzi jamii kuweza kutoa taarifa za watu walioingia na viashiria vya magonjwa.