Tanzania:Sampuli zilizochukuliwa hazijathibitisha uwepo wa virusi vya Murburg

Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema mpaka January 15, 2025, majibu ya uchunguzi wa kimaabara kutoka kwa Wahisiwa wa Ugonjwa wa Marburg waliochukuliwa sampuli hizo hayajathibisha uwepo wa virusi hivyo.

Taarifa hiyo imekuja siku moja tu tangu Shirika la Afya Duniani kutoa wasiwasi wake juu ya kushukiwa kwa virusi hivyo katika mkoa wa Kagera.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama kupitia taarifa yake amesema Serikali inachukua hatua za haraka ikiwemo kuimarisha mifumo ya ufatiliaji kuhusu mlipuko wa Ugonjwa huo.

“Wizara inapenda kuwahakikishia Wananchi pamoja na Jumuiya ya kimataifa, likiwemo Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation – WHO), kuwa imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na itaendelea kutoa taarifa zaidi”

Shirika  la Afya duniani, WHO, Januari 15,2025 liliripoti uwezekano wa kuweko kwa mlipuko wa homa ya Marburg wilayani Biharamulo na Muleba, mkoani Kagera nchini Tanzania baada ya watu 9 kuugua wakiwa na dalili zinazofanana  za ugonjwa huo ambapo kati yao 8 wamefariki dunia.

Kupitia ukurasa wake WHO imesema hadi tarehe 10 mwezi huu kulikuwa na wagonjwa 6 lakini idadi iliongezeka na kufikia 9 tarehe 11 mwezi huu na wagonjwa walikuwa na dalili kama vile maumivu ya kichwa, homa, maumivu ya mgongo, kuhara, kutapika damu, uchovu wa mwili na mwishoni kabisa ni kutoka damu kwenye matundu yote ya mwili.

Ikumbukwe kuwa iwapo itathibitika kwamba kuna mlipuko wa ugonjwa huo itakua ni mara ya pili nchini ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni Machi 16,2023 Serikali ilipotangaza ugonjwa usiojulikana katika katika Kata ya Maruku na Kanyangereko mkoani Kagera ambapo watu 9 waliathirika na Ugonjwa huo.

Homa ya Marburg huambukizwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu mwingine kupitia majimaji au damu ya mtu aliye na virusi hivyo.