Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema msaada wa chakula uliotolewa na wizara ya Kilimo ya Marekani kwa ushirikiano na Taasisi za Jumuiya ya Kimataifa katika baadhi ya shule za mkoa wa Dodoma ulifuata taratibu za uingizwaji wa chakula nchini.
Taarifa ya TBS iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa chakula hicho kilipoingizwa nchini kilifanyiwa ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa matumizi.
TBS imetoa taarifa hiyo kufuatia taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na msaada wa mchele ulioongezwa virutubishi, mafuta ya kupikia yaliyoongezwa virutubishi na maharage vilivyotolewa na taasisi hizo za nchini Marekani kupitia mpango wa Pamoja Tuwalishe.
Aidha, TBS imesisitiza kuwa utaratibu wa kuongeza virutubishi kwenye chakula unakubalika kitaalamu na hufanyika kwa lengo la kuboresha hali ya lishe kwa walaji.