TCAA:Ndege kushindwa kutua kwa sababu ya hali mbaya ya hewa ni jambo la kawaida

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Tanzania(TCAA) imethibitisha kushindwa kutua kwa Ndege ya Shirika la Ndege nchini humo (ATCL) yenye namba 5H-TCK katika uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera baada ya kuwepo hali mbaya ya hewa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hamza Johari imeeleza kuwa Ndege hiyo imeshindwa kutua katika uwanja huo kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa iliyohusisha mvua kubwa na kutanda kwa ukungu katika uwanja huo.

Ndege hiyo ambayo ilikuwa inaenda mjini Bukoba kupitia Mwanza ikitokea Dar es Salaam, ililazimika kutua salama katika uwanja wa Ndege wa Mwanza majira ya saa 6:56 mchana baada ya kushindwa kutua kwenye uwanja wa Bukoba

Hapo jana kupitia ukurasa wake wa twitter mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira aliandika “Still shaken lakini Mungu ni Mwema. Nimepanda ndege asubuhi ya leo kwenda Bukoba. Safari ilikuwa na changamoto, tumefika lakini ndege ikashindwa kutua. Nampongeza Rubani kwa uamuzi sahihi wa kurudi Mwanza na sasa narudi Dar. Serikali ibebe kwa uzito suala la airport mpya Bukoba”, ameandika Lugangira.

Johari ameeleza kwamba suala la ndege kuahirisha kutua au kufuta safari kwa sababu ya hali mbaya ya hewa ni jambo la kawaida katika usafiri wa anga na linaweza kutokea katika kiwanja chochote cha ndege ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema hata kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere wakati mwingine ndege hulazimika kuahirisha safari na kwenda kutua kwenye kiwanja mbadala au kufuta safari kwa sababu ya hali mbaya ya hewa: