Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema idadi ya wananchi wanaotumia huduma za kifedha kwa Mtandao wa simu imeendelea kuongezeka baada ya takwimu zao kuonyesha ongezeko la watumiaji huduma hizo hadi mwezi Septemba mwaka huu.
Taarifa ya utendaji kazi ya Mamlaka hiyo kwa mwaka 2022/23 inaonyesha kuwa akaunti za pesa kwa simu za mkononi zimeongezeka na kufikia watumiaji 39,590,502 mwezi Septemba mwaka huu kutoka watumiaji 35,201,960 walioripotiwa Mwezi Januari mwaka 2022.
Akizungumzia ongezeko Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari alisema kuwa Tanzania inazidi kuendeleza mfumo jumuishi wa kifedha kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wanaofanya miamala kupitia simu za mkononi.
“Takwimu za mawasiliano za mwezi Septemba 2022 zinaonyesha kwamba huduma za pesa kupitia simu za mkononi zimeongezeka kwa mfano idadi ya miamala imeongezeka kutoka bil. 349,952,830 hadi miamala bil. 366,178,409 Septemba 2022,” alibainisha Dkt. Jabiri.
Aidha, TCRA ilisema kuwa, akaunti za pesa kwa simu zimeongezeka kwa asilimia 1.5 katika miezi tisa iliyopita;kuanzia Januari hadi Septemba 2022; wakati miamala ikiongezeka kwa asilimia 2.
Mamlaka hiyo yenye dhamana ya kusimamia huduma za Mawasiliano nchini Tanzania ilibainisha kuwa, Januari mwaka huu watumiaji wa huduma za kifedha kwa Mtandao walikuwa 35,201,960 waliofanya jumla ya miamala 308,569,751 yenye thamani ya Shilingi 10,350,248,535,456 ikilinganishwa na watumiaji 39,590,502 waliofanya jumla ya miamala 366,178,409 yenye thamani ya Shilingi 12,722,059,888,707.
Mchanganuo wa Taarifa hiyo unaonyesha kuwa, Vodacom iliongoza katika soko kwa idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha ikiwa na asilimia 39 ya akaunti za fedha za simu na TTCL ‘ilifunga mraba’ ikiwa na asilimia 4.
Kwa mantiki hiyo idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha kwa kila Mtandao wa simu ilionyesha kwamba Vodacom hadi Septemba mwaka huu uliongoza kwa kuwa na idadi ya juu zaidi ya akaunti za kifedha zinazotumika zikirekodiwa kufikia watumiaji (15,554,527) Tigo (9,916,612), Airtel (8,955,102), Halotel (3,579,771) na TTCL ilihitimisha ikiwa na watumiaji wa huduma za kifedha (1,584,490).