The Chanzo yaondoa maudhui ya Askofu Gwajima kufuatia wito wa TCRA

Chombo cha habari mtandaoni, The Chanzo, kimetangaza kuondoa maudhui ya video iliyokuwa ikimuonesha Mbunge wa Kawe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Askofu Josephat Gwajima, kufuatia wito uliotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katika video hiyo, Askofu Gwajima, ambaye pia ni kiongozi wa dini, alizungumza na wanahabari tarehe 24 Mei, 2025, akitoa maoni kuhusu mfululizo wa matukio ya utekaji yanayodaiwa kutokea nchini Tanzania. Maudhui hayo yalichapishwa kwenye chaneli ya The Chanzo Online TV kupitia YouTube.

Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wao wa X (zamani Twitter), The Chanzo ilieleza kuwa imechukua hatua ya kuondoa video hiyo kwa mujibu wa agizo la TCRA, likieleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda uwazi na kuendeleza imani ya wasomaji na wadau wao.

Sehemu ya taarifa hiyo inasomeka:

“Kutokana na mazungumzo hayo kuendelea kufuatiliwa, ili kuboresha uwazi na imani ya wafuatiliaji wetu, The Chanzo inapenda kuwajulisha wasomaji na wadau wake wengine kuwa imetubidi kuyaondoa maudhui hayo kutokana na wito huo.”

Kwa mujibu wa barua ya TCRA, maudhui hayo yalikiuka misingi ya uandishi wa habari kwa kukosa mizania, kwa kuwa hayakuwapa nafasi mamlaka za serikali kutoa majibu kuhusu madai yaliyotolewa na Gwajima, hasa kuhusu idadi ya watu waliodaiwa kutekwa. TCRA ilieleza kuwa:

“Kitendo cha The Chanzo Online TV kupakia taarifa zenye kuegemea upande mmoja kinaweza kuhamasisha au kuchochea chuki dhidi ya Serikali kutoka kwa wananchi wake.”

The Chanzo ilibainisha kuwa licha ya kuwa ni nadra kupokea maelekezo ya aina hiyo, leseni yao ya maudhui iliwalazimu kuchukua hatua hiyo, ambayo ilitekelezwa rasmi leo Mei 27, 2025 saa 4:09 asubuhi.

-Alichozungumza Askofu Gwajima-

Katika mkutano huo wa Mei 24, Askofu Gwajima alitoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ndani ya taasisi za ulinzi na usalama, akisisitiza haja ya kuwa na mfumo huru wa uteuzi wa viongozi wa vyombo hivyo ili kuepusha ushawishi wa kisiasa.

Alieleza kuwa uhusiano kati ya siasa na vyombo vya dola unaathiri utendaji kazi wa vyombo hivyo, na hivyo kudhoofisha ufanisi wake katika kukabiliana na vitendo vinavyotishia usalama wa taifa.

“Ushauri wangu, wakuu wa vyombo vya usalama ili wafanye kazi zao kwa umahiri, wasiondolewe kwenye kazi zao kwa mapenzi ya mwanasiasa aliyewaweka. Hii itawapa uwezo wa kukataa baadhi ya maagizo yasiyo na maslahi kwa nchi,” alisema.

Gwajima pia alilaani vikali vitendo vya utekaji vinavyoripotiwa nchini, akieleza kuwa tayari kuna zaidi ya watu 80 wanaodaiwa kuwa walitekwa katika miaka ya hivi karibuni. Alisema baadhi yao walichukuliwa mbele ya familia zao, huku wengine wakipotea au kurudishwa wakiwa wamejeruhiwa au wamepoteza maisha.

“Utekaji si utamaduni wa Tanzania. Tumeona watu wanachukuliwa mbele ya familia zao, wengine wanapotea, wengine wanarudishwa wakiwa wamejeruhiwa au wamepoteza maisha. Hili si jambo dogo na linaumiza taifa,” alisema Gwajima 

Aidha, aliongeza kuwa ingawa ni mwanachama wa CCM, hatakuwa tayari kunyamaza mbele ya matendo yanayokiuka haki za binadamu na utu.

“Anayesema napinga CCM nimwulize, je, CCM tunakubali utekaji? MwanaCCM wa kweli lazima apinge jambo hili.”

Gwajima alikosoa pia kauli zinazohusisha matendo hayo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akisema zinachafua taswira ya Rais na kuhatarisha uhusiano wa kidiplomasia.