Kenya siku ya Jumatatu ilianzisha kampeni ya kusajili wapiga kura wapya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, huku vijana wakitumia video za TikTok na muziki kupunguza hali ya kukata tamaa miongoni mwa wenzao.
Mnamo Juni 2024, wimbi la maandamano lililoongozwa na kile kinachoitwa “Gen Z” lilienea nchini baada ya Rais William Ruto kutangaza ongezeko la kodi, jambo lililopunguza umaarufu wake miongoni mwa vijana.
Maandamano hayo yaliongezeka na kuwa machafuko makubwa zaidi yakihusisha masuala ya ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100 na wengine kadhaa kutoweka, kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Ingawa maandamano hayo yamepungua, vijana wengi bado wamekatishwa tamaa na utawala wa Ruto, ambao uliingia madarakani kwa ahadi ya kuwainua vijana na maskini.
“Watu wanateseka, watu wanakufa. Fedha zinapotea tu bila maelezo,” alisema Mark Kipchumba mwenye umri wa miaka 21, akieleza hali ngumu ya kiuchumi na ufisadi uliokithiri kama sababu ya kujisajili kwa mara ya kwanza kupiga kura.
Kampeni ya siku 30 ya usajili wa wapiga kura iliyoanzishwa na Independent Electoral and Boundaries Commission inalenga kusajili angalau wapiga kura wapya milioni 2.5 katika awamu ya kwanza.
Tume hiyo inasema inalenga kuongeza wapiga kura wapya milioni 6.3 kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao, ambapo asilimia 70 wanatarajiwa kuwa vijana.
“Niko hapa kwa sababu ya matumaini ambayo kadi hii inaleta kwa ajili ya siku zijazo,” alisema Peter Mwangi mwenye umri wa miaka 22, mwanafunzi wa filamu katika chuo cha Multimedia University of Kenya, akizungumza na AFP.
Licha ya idadi ndogo ya sasa, kampeni inayoongozwa na vijana iitwayo #NikoKadi (Nina kadi ya mpiga kura) inaendelea kugeuza usajili wa wapiga kura kuwa jambo la kuvutia kwa kuhamasisha vijana kujisajili.
TikTok, muziki na mbinu bunifu

Kuanzia video za TikTok hadi biashara zinazotoa punguzo kwa waliojisajili, pamoja na tamasha la muziki lililopangwa kufanyika Mei ambapo kadi ya mpiga kura itahitajika kuingia, vijana wanatumia mbinu za ubunifu kuongeza usajili.
Mwanaharakati Ademba Allans, mwanzilishi wa kampeni ya #NikoKadi, anasema uhamasishaji unaendelea kushika kasi, lakini akaongeza kuwa, “kukata tamaa ni mojawapo ya changamoto kuu tunazojaribu kupambana nazo.”
Uchaguzi wa Kenya wa mwaka 2022 ulikuwa na idadi ndogo zaidi ya wapiga kura katika kipindi cha miaka 15, ambapo vijana ambao ni sehemu kubwa ya idadi ya watu walichangia asilimia 39.8 pekee ya wapiga kura waliosajiliwa, ikiwa ni punguzo la alama 5.2 kutoka mwaka 2017.
Allans anatarajia kubadilisha hali hiyo pamoja na siasa za taifa hilo la Afrika Mashariki, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitawaliwa na wanasiasa wanaoonekana kutokuelewa maisha halisi ya vijana wa Kenya.
“Tunataka kubadilisha mfumo. Tunataka kuwaondoa wote walioko serikalini,” alisema kijana huyo wa miaka 26.
Velma Omondi mwenye umri wa miaka 22 alisema aliwatishia marafiki zake wawili “kuachana nao” iwapo hawangejisajili na walifanya hivyo.
“Niliwapa sharti,” alisema. na kuongeza“Hatuwezi kudai mabadiliko ikiwa hatuko tayari kushiriki katika mabadiliko hayo,”