Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi leo Jumanne Februari 18, 2025, kwenye Uzinduzi wa kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Jijini Mwanza, ameshauri kuzingatiwa kwa Ibara ya Tisa ya Katiba ya Tanzania yenye kuhimiza kuhusu utu, Upendo na utii kama suluhu ya migogoro mingi ya kijamii.
Wakili Mwabukusi ametoa kauli hiyo kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Chama cha sheria Tanzania, akishukuru pia kwa huduma hiyo ya msaada wa kisheria kwa namna ambavyo imekuwa mkombozi kwa wananchi wanyonge wasiokuwa na uwezo wa kulipa Mawakili kwenye kuwasimamia mahakamani
Akisisitiza kuhusu misingi hiyo ya Utu, utii na Upendo, Mwabukusi amesema ni muhimu kuzingatiwa kwa mambo hayo bila kujali nafasi ya mtu kwenye jamii akisema kudhorota ama kufa kwa mambo hayo ndipo kunakosababisha migogoro ya ndoa, ardhi pamoja na mashauri mengi ya mirathi kuwepo mahakamani na migogoro ya kijamii.
Ametumia sehemu ya hotuba yake pia kuwaalika wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kupata msaada huo wa kisheria, akisema Chama Cha Wanasheria nchini TLS kipo kwaajili ya wasiokuwa na sauti na kimejipanga kikamilifu kuhudumia wananchi kupitia kampeni hiyo ambayo leo imeingia kwenye Mkoa wa kumi na nane.