Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Ziwa Magharibi, imefanikiwa kukamata aina 34 za dawa zenye thamani ya shilingi 4,235,100 zikiuzwa kinyume cha sheria ya dawa na vifaa tiba.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Meneja wa TMDA, Kanda ya Ziwa Magharibi Ofisi za Geita, Dk Edgar Mahundi wakati akikabidhi dawa hizo kwa mkuu wa mkoa wa Geita mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Dk. Mahundi amesema dawa hizo zimekamatwa katika msako uliofanywa kwenye jumla ya halmashauri tisa za mikoa ya Geita, Kagera na Shinyanga kwa kipindi cha mwezi Julai mwaka 2021 hadi Januari 2022.
“Dawa hizi zimeondolewa kwenye hayo maeneo, kwa sababu baadhi ya maeneo hayajasajiliwa kuuza aina hiyo ya dawa, lakini pia dawa hizi ni dawa moto, wauzaji waliokutwa nazo walikuwa hawana sifa ya kuuza hizi dawa.
“Dawa hizi ni zile ambazo zinatakiwa zitolewe kwa maelekezo maalumu ya kitaalamu, kwa hiyo hapa utakuta kuna dawa za kutibu presha zipo, dawa za kisukari zipo, dawa za kuzuia ujauzito zipo, dawa za minyoo zipo.
“Dawa hizi zinatakiwa ziwepo kwenye maduka makubwa ya dawa au kwenye hospitali zenye watalaamu, mahala zilipokutwa hizi dawa zimeondolewa kwa sababu wamevunja sheria ya dawa na vifaa tiba sura 219,” amefafanua.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameagiza maduka yote ya dawa kuzingatia kanuni na sheria ya dawa na vifaa tiba na kuagiza wote wanaokiuka kuchukuliwa hatua, ili kuepuka madhara ya kiafya kwa watumiaji.