Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema ndani ya miezi minne limesafirisha zaidi ya abiria 1,000,000 kupitia treni yake ya kisasa ya SGR, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya waliokuwa wanasafirishwa na treni za zamani kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa ya TRC iliyotolewa leo idadi hiyo ni mara mbili ya waliosafiri na treni ya zamani ya (MGR), ambayo ilisafirisha jumla ya abiria 400,000 katika kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha TRC imesema inatambua umuhimu wa huduma hiyo ya kisasa katika kuboresha usafiri, kuongeza ufanisi wa biashara na kutoa chaguo la haraka na salama kwa abiria hivyo imewataka wananchi kulinda miundombinu ya reli hiyo.
Ikumbukwe kuwa safari za treni hiyo zilianza rasmi Julai 14,2024 kwa kutokea Dar es salaam hadi Morogoro na kisha baadae kuongeza kutoka Dar es salaam hadi Dodoma.