Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
TRC yatoa ufafanuzi mabehewa mapya ya reli ya kisasa - Mwanzo TV

TRC yatoa ufafanuzi mabehewa mapya ya reli ya kisasa

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema mabehewa yote yaliyoainishwa kuletwa kwa ajili ya treni ya Reli ya Kisasa (SGR) yatakuja na kwamba yaliyoanza kuingia nchini ni ya safari ndefu.

Wiki hii katika mitandao ya jamii kumekuwa na picha zikionyesha mabehewa yaliyoletwa sio yale yaliyoahidiwa kuletwa nchini kutokana na tofauti ya muonekano wake.

Leo Alhamis Novemba 24, 2022, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amezungumza hayo wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea ujenzi wa SGR katika eneo la Kikuyu jijini Dodoma.

“Tayari tumeanza kupokea mabehewa 14 ya abiria kwa ajili ya uendeshaji wa kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro,”amesema.

Amesema picha zinazosambaa katika mitandao ya jamii zinaonyesha mabehewa hayo ambayo yatapokelewa rasmi kesho Ijumaa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Kadogosa amesema picha ya mchongoko zinazoonyeshwa katika mitandao hiyo ni za treni ambazo zitatumika kwenye safari za mda mfupi na kwamba treni hizo zitawasili Juni 2023.

Amesema safari za treni ya SGR kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro zitaanza Februari 2023.

Aidha, Kadogosa amesema taarifa kuwa kuna mabehewa yatapigwa mnada sio za kweli na kwamba TRC haihusiki na hilo.

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imelenga kuimarisha sekta ya usafirishaji ili kupanua uchumi wa mtu mmoja na Taifa kwa kuwezesha watu wanaofanya shughuli zozote za kiuchumi kupata usafiri.

“Hapa Dodoma kutajengwa bandari kavu kubwa sana, eneo la kuweka mizigo kutoka bandarini litakuwa hapo…nataka niwahakikishie usimamizi huu wenye maelekezo ya mkuu wa nchi, sisi tuliopewa dhamana ni kufikia malengo,” alisema.