Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kujadiliana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini humo (TUCTA) kuhusu hoja ya wafanyakazi ya nyongeza ya mishahara.
Hapo jana Viongozi wa Tucta wakiwa jijini Dodoma walisema kuwa leo watawasilisha serikalini hoja zao kwa maandishi na wakasema hawataondoka Dodoma hadi suala hilo litakapofikia tamati au kuwa na sura nzuri ya utekelezaji.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), nchini Tanzania bwana Gerson Msigwa aliwaeleza wanahabari jijini humo kuwa tayari serikali imeanza majadiliano ya awali na Tucta.
“Serikali iliahidi itatoa ufafanuzi juu ya hoja za wafanyakazi kuhusiana na nyongeza ya mshahara wa kima cha chini, leo (jana) tumekutaka na viongozi wa vyama vya wafanyakazi vinavyounda Tucta. Baada ya mazungumzo wameomba wakamilishe majadiliano yao watakutana na serikali ili tusikilize hoja zao kwa majadiliano,” alisema.
Msigwa alisema viongozi wa Serikali walioshiriki majadiliano hayo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Deogratius Ndejembi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Laurean Ndumbaro na wataalamu kutoka wizarani.
Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alisema: “Leo (jana) viongozi tulikutana na Serikali kwa ajili ya mjadala juu ya ongezeko la mshahara kwa watumishi wa umma. Tunashukuru viongozi wa serikali wamefika akiwamo waziri, katibu mkuu na wataalamu wao. Tumezungumza na tumeonesha ni kwa kiwango gani watumishi na sisi viongozi wao hatujaridhika na utaratibu wa nyongeza za mshahara ulivyofanyika.” Aliongeza:
“Leo(jana) tumeweza kuonesha kuwa kilichofanyika hatukukitegemea. Hiyo nyongeza ya asilimia 23.3 iliyotangazwa na Mheshimiwa Rais ingewagusa watumishi wenye vima vyote vya mishahara kwa kiwango kilichozoeleka na kwa bahati mbaya kiwango kimekuwa cha chini ambacho kwa kweli kimewaumiza sana wafanyakazi wa nchi hii.”
Nyamhokya alisema baada ya kufikisha mapendekezo watasubiri serikali iyafanyie kazi hasa ikizingatia Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kutekeleza nyongeza hiyo katika bajeti inayoanza Julai mwaka huu.
“Wafanyakazi walikuwa na shauku, lakini kwa bahati mbaya kilichotokea ni tofauti. Sisi tuko Dodoma kwa jambo hili naamini tutanyanyua mguu kutoka hapa jambo hili likiwa limefikia tamati au angalau limeleta sura nzuri,” alisema