Tume yabaini mbinu 16 zilizotumika kuratibu ghasia za Oktoba 29

Ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania imebainisha kuwa takribani mbinu kumi na sita zilitumika katika kuandaa, kuratibu na kutekeleza ghasia na vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa ripoti hiyo mbele ya Rais, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande, amesema mbinu hizo zililenga kuathiri shughuli za uchaguzi na kusababisha taharuki katika maeneo mbalimbali nchini.

Tume imeeleza kuwa miongoni mwa mbinu zilizotumika ni pamoja na kuweka vizuizi barabarani, kuchoma moto, matumizi ya alama na ishara za kutambuliana kati ya wahusika, matumizi ya pikipiki kwa harakati za haraka, pamoja na kufanya vurugu kwa wakati mmoja katika maeneo mengi ili kuvuruga udhibiti wa usalama.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tume imepata ushahidi unaoonyesha kuwa matukio hayo hayakutokea kwa bahati mbaya, bali yalipangwa, yaliratibiwa, yalifadhiliwa na kutekelezwa na watu waliokuwa na maandalizi ya awali, ikiwemo kupata mafunzo maalum.

Waratibu wa matukio hayo wanadaiwa kutumia mbinu ya kuwasajili vijana katika maeneo mbalimbali, wakiwemo vyuo vikuu, masoko na vituo vya mabasi, kwa lengo la kuwashawishi kushiriki katika ghasia za Oktoba 29.

Tume imeeleza kuwa baadhi ya waratibu hao hawakukamatwa kutokana na kutokuwepo kwao wakati wa utekelezaji wa vurugu hizo.

Ripoti imebainisha kuwa kulikuwa na vichocheo vikuu vitatu vilivyochangia kuibuka kwa ghasia hizo.

Kwanza ni matumizi ya mitandao ya kijamii, ambapo kabla na baada ya uchaguzi, mitandao hiyo ilitumika kusambaza ujumbe wa kuhamasisha watu kutoshiriki uchaguzi au kuhakikisha haufanyiki kabisa.

Pili ni matumizi ya kauli mbiu na matamko ya kisiasa, ambapo baadhi ya wanasiasa walitumia kauli kali kama “no reform no election”, “Oktoba hatutiki”, “Samia Must Go”, na “hakuna uchaguzi bila mabadiliko ya mfumo”, ambazo Tume inasema zilichochea hisia za uhasama na kuhamasisha vurugu.

Tatu ni baadhi ya wanasiasa katika maeneo mbalimbali ambao, kwa mujibu wa Tume, walitumia mazingira ya kisiasa kujinufaisha, hususan wagombea wa ubunge na udiwani, kwa kuhamasisha wafuasi wao kushiriki katika ghasia kwa matumaini ya kupata mabadiliko ya mfumo wa kisiasa.

Tume imehitimisha kuwa ghasia za Oktoba 29 hazikutokea bila mipango, bali zilichochewa na mtandao wa mbinu mbalimbali za kimkakati zilizolenga kuvuruga mchakato wa uchaguzi.

Ripoti hiyo imependekeza hatua za kuimarisha usimamizi wa usalama, udhibiti wa taarifa mitandaoni, na uwajibikaji wa wadau wa kisiasa ili kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo katika siku zijazo.