Tundu Lissu ailalamikia Mahakama, ni kuhusu watu wake kuzuia na kufukuzwa nchini

Leo, Mwenyekiti wa CHADEMA anayekabiliwa na kesi ya uhaini, Tundu Lissu, aliendelea kulalamikia vizuizi vinavyowakabili watu wake kuingia mahakamani ili kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo. 

Katika maelezo yake mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastun Ndunguru, Lissu alisema kuwa baadhi ya watu waliokuwa tayari kushiriki katika kusikiliza kesi hiyo, wakiwemo raia wa kigeni, walifukuzwa nchini na kurudishwa nchini mwao.

Akielezea kuhusu tukio hilo, Lissu alisema:

“Watu hawa walikuja kushiriki katika kesi hii kwa lengo la kuona jinsi taratibu za mahakama zinavyoendelea. Lakini badala ya kuruhusiwa kuingia, walizuiliwa hadi lango la Mahakama Kuu. Baada ya kuzungumza na Naibu Msajili ambaye aliwahakikishia kuwa angewasaidia, walichukuliwa na maafisa wa uhamiaji na kupelekwa kwenye ofisi za uhamiaji. Hatimaye, walifukuzwa nchi hii ili wasiweze kushiriki.”

Jana Oktoba 14, 2025 Idara ya Uhamiaji nchini ilisema imelazimika kuwaondosha nchini Tanzania Raia wawili wa kigeni ambao ni Dkt. Brinkel Stefanie mwenye hati ya kusafiria ya Ujerumani namba C475MMNGL na Catherine Janel Almquist Kinokfu mwenye hati ya kusafiria ya Marekani namba A80321764 baada ya kubainika kuwa wamekiuka masharti ya viza zao za matembezi.

Kufuatia tukio hilo, Msemaji wa Idara ya Uhamiaji kupitia Ofisi ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Jijini Dodoma, SSI. Paul J. Mselle ametoa wito kwa Raia wa kigeni wanaoingia na kuishi nchini kwa madhumuni mbalimbali kuzingatia matakwa yaliyoainishwa katika viza au vibali vyao kwa mujibu wa sheria ya uhamiaji sura 54 pamoja na kanuni zake ili kuepuka usumbufu

Lissu alisisitiza kuwa tukio hili ni la kinyume na kanuni za kisheria na haki za msingi za binadamu, na ni sehemu ya kadhia kubwa iliyotokea katika mahakama. 

Aliongeza “Hii si mara ya kwanza. Hii ni mara ya tatu kwa watu kujaribu kuja nchini kushiriki katika kesi hii na kufukuzwa. Kesi ilianza na wananchi wa Kenya, ikafuata wale wa Kisutu walioweza kuingia, na sasa hali hii imetokea kwa raia wa Ujerumani na Marekani waliokuja kwa lengo la kushiriki kesi.”

Lissu alibainisha kuwa kesi hii ni kubwa zaidi kuliko kesi nyinginezo zote zilizowahi kushughulikiwa, na kwamba baadhi ya watu waliozuiliwa wameshapokelewa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika. Alisisitiza:

Kadhalika Lissu katika kusisitiza na kujenga msingi wa hoja zake  alirejea kesi mbalimbali zenye ukubwa unaofana na yake ambazo viongozi mashughuli walikabiliwa nazo, akisema katika kesi hizo wapo raia w kigeni walihudhuria bila masharti yoyote kwa kuwa zilikua na mvuto kwa umma.

“Ukikagua historia ya kesi nchini, mwaka 1958 kulikuwa na kesi kubwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dar es Salaam, Kivukoni Rejina dhidi ya Nyerere na wenzake wawili, ambayo ilihusu tuhuma za uchochezi.Hata wakati huo, wakoloni hawakuwahi kuzuia watu kuingia mahakamani, na Mwalimu Julius Nyerere aliteteiwa na wakili kutoka Uingereza bila kuingiliwa. Vilevile, mwaka 1959 kulikuwa na kesi ya uhaini nchini Afrika Kusini, ambapo hali ilikuwa hatari, lakini hakuna mtu aliyefukuzwa au kuzuia watu kushiriki mahakamani.”

Akizungumza kuhusu hali ya sasa, Lissu alisema:

“Baada ya miaka 64 ya uhuru, serikali ya Tanzania pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama inaonekana kufanya vitendo vya ukandamizaji, kuogopwa na kuzuia wananchi kushiriki katika taratibu za kisheria. Matendo haya yamezidi yale ya wakoloni, na mara nyingine yanazidi ukatili uliotendwa na wakoloni.”

Mlalamikaji huyo, ambaye kwa sasa yupo gerezani, alisisitiza kwamba hana uwezo wa kuchukua hatua nyingine zaidi ya kutoa taarifa, ili kuhakikisha haki inatendeka. Aliongeza:

“Mahakama yenyewe haijafanikiwa kuhakikisha kuwa watu wanaweza kushiriki kusikiliza kesi. Hatuwezi kukaa kimya pale ambapo kesi muhimu kama hii inashughulikiwa na majaji. Watu wanastahili kushiriki, na hakuna mbadala zaidi ya kuzungumza ili kulinda haki.”

Lissu alihitimisha kwa kuonya kwamba kuzuia raia kushiriki kwenye kesi zinazohusu masuala makubwa ya kisheria ni hatari kwa mfumo wa mahakama na ni kinyume na kanuni za haki na uwazi. Alisisitiza umuhimu wa kuruhusu kila mmoja kushiriki ili kuhakikisha haki inatendeka kikamilifu, na kuonyesha kuwa historia ya kisheria inapaswa kuheshimiwa.