Katika kile kinachoonekana kuwa ni hatua ya kipekee na yenye uzito wa kikatiba na kisheria, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki na mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, Tundu Antiphas Lissu, ameiambia Mahakama kuwa hataki wakili yeyote kumwakilisha katika kesi yake ya uhaini, akisisitiza kuwa ataendelea kujitetea mwenyewe.
Lissu alitoa kauli hiyo leo mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, akifafanua kuwa uamuzi huo umetokana na uzito wa kesi hiyo, ambayo endapo atapatikana na hatia, adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
“Sio kwamba sikumtambua au sikumfahamu, lakini alikuja mwenyewe gerezani Ukonga na kuniambia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa kuniwakilisha,” alisema Lissu akimrejelea Wakili Neema Saron aliyeteuliwa na Mahakama. “Nilimjulisha wazi kwamba kwa kesi ya aina hii, yenye kosa la adhabu ya kunyongwa, mimi mwenyewe nitajitetea.”
Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai chini ya kifungu cha 329 inampa haki mshtakiwa kupewa uwakilishi kwa maana ya Wakili ambaye anateuliwa na Mahakama kwa ajili ya kumwakilisha iwapo hana uwezo wa kumudu gharama za kisheria ama hana mawakili.
Hata hivyo Lissu ameishukuru Mahakama kwa kuweza kumpatia Wakili huku akisema hajashindwa kulipa gharama za mawakili kwani tayari alikua na jopo la mawakili lililokuwa likimwakilisha hapo awali wakati mwenendo wa kesi ulipoanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
“Naomba niwape shukrani kwa kunifikiria na kuniteulia wakili. Pamoja na kwamba sikumuomba, na sikumfahamu, lakini nawashukuru kwa juhudi zenu. Hata hivyo, kwa kesi hii ya uhaini, nitajitetea mwenyewe.”
Lissu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA alisema amekuwa na msimamo huo tangu mwanzo wa shauri hili, na amekuwa akiieleza Mahakama kuwa hataki mtu mwingine azungumze kwa niaba yake.
“Najua haki ya mshtakiwa kuwa na uwakilishi wa kisheria iko wazi, hata kama hana pesa ya kumlipa wakili. Lakini kwa kesi kama hii, ni muhimu mimi mwenyewe kuzungumza. Huu ni mtihani wa kikatiba na wa haki za binadamu – kwamba mtu anaweza kushtakiwa kwa maneno aliyoyasema, na kama akikutwa na hatia, anyongwe.”
Kadhalika Lissu aliiomba Mahakama ikiwa itakubali kuwaingiza jopo la Wanasheria watakaomsaidia kufanya tafiti za kisheria kwenye rekodi rasmi za Mahakama kutokana na kwamba yeye hawezi kupata baadhi ya taarifa kwa kuwa yupo gerezani.
Upande wa Jamhuri ulijibu hoja hiyo kwa kusema kuwa kifungu cha 329 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinampa mshtakiwa haki ya kuwa na wakili au kujitetea mwenyewe kwa hiari. Kwa kuwa Lissu ameeleza wazi kuwa atajitetea, upande wa mashtaka hauna pingamizi na unaheshimu uamuzi huo.
Hata hivyo, Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga alieleza kuwa Jamhuri inapinga maombi ya mawakili waliokuwa tayari kusaidia kwa kufanya utafiti (“research”) wa kisheria kwa ajili ya Lissu, kuingizwa rasmi kwenye rekodi ya Mahakama kama sehemu ya timu ya utetezi.
“Sisi hatupingi wao kumsaidia nje ya Mahakama, lakini tunapinga kuingizwa kwao kwenye rekodi rasmi ya Mahakama kwa sababu hilo linaweza kuleta mkanganyiko wa kisheria.”
Mahakama, baada ya kusikiliza hoja hizo, ilikubaliana na msimamo wa Lissu wa kujitetea mwenyewe na kusema iwapo mawakili wataendelea kuwa sehemu ya timu ya utafiti wa Lissu bila kuingia kwenye rekodi, hilo litakuwa suala la ndani ya utetezi.
Mbali na hoja ya uwakilishi, Lissu pia aliwasilisha pingamizi kuhusu mamlaka ya Mahakama Kuu kusikiliza kesi hiyo, na Hatua za mwenendo mzima wa shauri lake akidai kuwa taratibu zilizotumika zilikuwa batili na kinyume cha sheria.
“Nilikamatwa Mbinga, Ruvuma, lakini nikasafirishwa usiku hadi Dar es Salaam na kufikishwa Mahakama ya Kisutu. Kisheria, kesi ya aina hii ya uhaini inapaswa kuwasilishwa kwenye Mahakama ya eneo nilikokamatwa,” alisema Lissu.
Akinukuu kifungu cha 261 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Lissu alisema kuwa hati ya mashtaka ya uhaini lazima iwasilishwe katika Mahakama Kuu ya eneo ambalo kosa linadaiwa kufanyika, na si vinginevyo.
-Mkanganyiko wa nyaraka-
Katika hatua nyingine, Lissu alieleza kuwa alipewa nakala ya nyaraka za kesi akiwa gerezani ambazo zinaonyesha kuwa mwenendo wa kesi ulianza tarehe 18 Oktoba, badala ya 10 Aprili kama ilivyo kwenye nyaraka rasmi za Mahakama.
Lissu analalamika kwamba nyaraka aliyopewa leo mahakamani ina tofauti na ile aliyopelekewa gerezani hivyo anasema kuna kosa limetendeka hivyo huenda ikawa ni kosa la jinai.
“Hizi nyaraka zinaonyesha jambo tofauti. Kuna uwezekano mkubwa kwamba jambo fulani limefanyika kinyume cha sheria – huenda ni kosa la jinai,” alidai Lissu.
Itakumbukwa kuwa kesi hiyo leo ililetwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja za awali kwenye kesi ya Uhaini inayomkabili kiongozi huyo mashuhuri.
Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Nduguru, Jamse Karayemaha, Ferdinand Kiwonde ndio wanaosikiliza shauri hilo
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Septemba 9,2025 saa nne asubuhi kwa ajili ya kuendelea kusikiliza hoja za mapingamizi zilizotolewa na Lissu na hatua nyingine za kisheria