Mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kwenye siasa nchini Tanzania, Tundu Lissu amerejea nchini baada ya kuwa uhamishoni kwa zaidi ya miaka 7 ikiwa ni wiki chache tu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mikutano ya kisiasa.
Lissu ambaye ni Makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliwasili majira ya Saa 7:30 mchana katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 3 akitokea nchini Ubelgiji alikokuwa akiishi.
Kiongozi huyo anayefahamika kwa kukosoa vikali Serikali iliyopo mamlkani alipokelewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakimsubiri nje ya uwanja huo wakitokea sehemu tofauti tofauti za Tanzania.
Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali na bendera za chama hicho, huku wengi wakisema “Mwamba amerudi”
Mara tu baada ya kuwasili, Lissu aliingia kwenye gari kisha kukaa juu yake huku akipunga mkono uliokuwa umeshika bendera ya Chadema kwa wafuasi wake waliokuwa wamejipanga barabarani na kufuata magari yaliyokuwa yameenda kumpokea.
Wakizungumza na Mwanzo TV kwa nyakati tofauti wanachama wa Chadema wamesema ujio wa Lissu nchini huenda ukabadili upepo wa siasa nchini.
Tangu kushambuliwa, huu sio ujio wake wa kwanza nchini Tanzania. Ila unaashiria utakuwa wa kudumu. Alirudi Tanzania kwa mara ya kwanza Julai 2020 – ili kushiriki kinyang’anyiro cha nafasi ya urais wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Uchaguzi uliomrudisha madarakani hayati John Pombe Magufuli, kabla ya kifo chake Machi 2021.
Tundu Lissu alirudi Ubelgiji Novemba 2020 baada ya uchaguzi kuisha. Safari ya kurudi haikuwa nyepesi. Alilazimika kwanza kukimbilia ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania kupata hifadhi, kwa kile alichoeleza usalama wake kuwa hatarini. Na sasa anarudi tena!
Lissu anatarajia kuhutubia katika mkutano wa hadhara utakaofanya viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam.