TWAWEZA:Tozo za miamala zinadhihirisha changamoto ya utawala

Matokeo  ya utafiti uliofanywa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya TWAWEZA  yameonesha kuwa maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu yanatofautiana lakini wengi wao wakisema tozo ni kubwa.

Kwa mujibu wa takwimu za matokeo hayo yaliyowasilishwa jana  jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TWAWEZA, Aidan Eyakuze ni kwamba asilimia 67 ya wananchi wengi wanakubali kuwa tozo hiyo ni njia muhimu ya serikali kukusanya mapato na asilimia 63 wanaamini kwamba inasaidia kumfanya kila mtu achangie maendeleo ya taifa.

Aidha, asilimia 46 wamekubali kuwa tozo hiyo itapunguza utegemezi kwa wafadhili ambapo asilimia 43 wamekubali tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu ni kitu zuri.

Akiwasilisha mukhtasari wa matokeo hayo, Eyakuze amesema wananchi wanaonesha dalili kuwa wangeunga mkono zaidi tozo hizo iwapo wangekuwa na taarifa kamili kuhusu matumizi ya fedha zinazokusanywa kupitia tozo.

“Asilimia 63 wanasema wangekuwa tayari zaidi kulipa tozo iwapo wangeweza kufuatilia matumizi ya fedha hizo. Asilimia 39 wanasema wanajua pesa zinatumikaje na asilimia 44 wanasema wanaweza kutafuta kwa urahisi taarifa kutoka serikalini juu ya matumizi ya mapato ya tozo.

Aidha, amesema wananchi wanataja miradi mbalimbali ambayo wangependa yanufaike na tozo za miamala. Eneo la kwanza kabisa ni huduma za afya (57%) na elimu (50%), ikifuatiwa na ujenzi wa barabara (38%), huduma za maji (33%), umeme (20%), kilimo (18%) na mikopo (17%) pamoja na maeneo mengine ambayo yametajwa kenye ripoti hiyo

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kwamba maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu yanadhihirisha changamoto ya utawala. 

Twaweza  imesema Serikali haina budi kupanua wigo wa kodi ili kuongeza mapato yatakayo gharamia huduma za jamii. Kupanua wigo wa walipakodi kunawashirikisha wananchi wengi zaidi kwenye mipango ya maedeleo na kuwafanya wadai uwajibikaji kwa serikali.

“Lakini huduma za fedha kwa njia ya simu zimesaidia sana kwenye biashara na mapato ya familia. Tozo zimepandisha gharama za huduma hizi muhimu, zimewafanya wananchi wapunguze kwa kiasi kikubwa matumizi ya huduma hizi na huenda zikaathiri ukusanyaji wa mapato,”

Utafiti huo  maalum wa Sauti za Wananchi wa awamu ya saba, ulifanyika kati ya Juni hadi Julai 2022, ambapo jumla ya waliohojiwa kwenye utafiti huo ni watu takribani 3000.

Sheria ya Tozo za Miamala ya Simu ya Kutuma na Kupokea kwa njia ya Kielektroniki ya 2021, ilianzisha tozo kwenye miamala ya pesa kwa simu kuanzia Julai 2021. 

Gharama hizo zilipunguzwa kwa 30% mwezi Septemba 2021 na zikapunguzwa tena mwezi Julai 2022, na hivyo kufanya punguzo la jumla la 60% ya kiwango cha kilichowekwa awali.