Ubalozi wa Tanzania nchini India umetoa ufafanuzi kuhusu Mtanzania, Sayuni Eliakim aliyedaiwa kushindwa kusaidiwa ubalozini hapo kupata hati ya kusafiria ili arudi Tanzania.
Ubalozi huo umetoa ufafanuzi ikiwa ni siku mbili tangu taarifa hizo zilizodai Sayuni aliyedaiwa kunyanyangâanywa hati ya kusafiria na mwenyeji wake kuwa alikosa huduma ubalozini hapo na kumtaka arudi ajaze maombi hayo kwa njia ya mtandao
Ufafanuzi huo umetolewa leo Jumatatu Agosti 28, 2023 na Balozi wa Tanzania nchini humo, Anisa Mbega ambaye amesema kuwa Sayuni alizidisha muda wa kibali chake cha ukaazi nchini humo, hivyo kuna ugumu katika mchakato wa kumrudisha Tanzania.
âSayuni Eliakim aliingia nchini India mwaka 2018, na kukaa kwa muda mrefu hadi kujikuta muda wake wa ukaazi umepita. Kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za uhamiaji za India, raia wa kigeni ambaye amepitisha muda wake wa ukaazi, haruhusiwi kutoka nchini India, isipokuwa kwa utaratibu maalum uliowekwa.
âUtaratibu huo ni pamoja na kuomba ruhusa ya kutoka nje ya nchi (Exit Permit). Maombi ya âExit Permitâ yanatakiwa kufanyika katika mji ambao mhusika anaishi (kwa upande wa Sayuni mji anaoishi ni Bangalore). Sayuni alielekezwa kuhusu utaratibu huo na maombi yake hadi hivi sasa yanaendelea kufanyiwa kazi,âamesema Balozi Anisa.
Balozi Anisa amesema wanaendelea kumsaidia Sayuni kwa kumpatia Hati ya Kusafiria ya Dharura (ETD).
Aidha, Ubalozi umetoa rai kwa Watanzania kujiepusha na kuchukua tahadhari na watu wasio waaminifu wanaowalaghai kuhusu kuwepo kwa nafasi za ajira zisizo na ujuzi kwa raia wa Tanzania nchini India.