Ubalozi wa Tanzania nchini Korea wakana taarifa ya Tanzania kusaini mkataba unaouza bahari na madini yake.

Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini umesema Tanzania haijasaini mkataba wowote na Jamhuri ya Korea unaohusu Bahari wala Madini katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan inayoendelea nchini humo.

Katika taarifa yake Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini,Togolani Mavura amesema kuwa katika ziara hiyo Rais Samia ameshuhudia utiwaji saini wa mkataba mmoja tu ambao ni wa mkopo wa masharti nafuu wa dola Bilioni 2.5 za Kimarekani kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Mbali na mkataba huo Rais Samia ameshuhudia utiwaji saini wa Hati za Maelewano mbili za Ushirikiano katika sekta za Uchumi wa Bluu na Madini ya Kimkakati.

Aidha, alishuhudia kusainiwa kwa tamko la Utayari wa Kuanza Majadiliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi.

Balozi huyo wa Tanzania nchini Korea Kusini ameongeza kuwa Tanzania haijagawa chochote kubadilishana na mkopo nafuu kutoka Korea Kusini kama ilivyoandikwa na chombo kimoja cha habari na kwamba Tanzania inapata mkopo wa masharti nafuu kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo (EDCF) kwa mara ya tatu.

Mara ya kwanza dola Milioni 733 za Kimarekani (2014-2020), mara ya pili dola Bilioni Moja (2021-2025) na huu mkopo wa tatu ni dola Bilioni 2.5 (2024-2028) ambapo nchi 59 za Afrika, Asia na Ulaya zinafaidika na mkopo wa aina hiyo kutoka EDCF.

Balozi Mavura amesema tofauti na ilivyoandikwa, mkopo huo wa masharti nafuu una riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una fungate ya miaka 25, ikimaanisha unaanza kulipwa baada ya mwaka wa 26.

Hivyo, amesisitiza si kweli kwamba mkopo huo utalipwa kwa miaka 5 na kwamba taarifa iliyotolewa na chombo hicho cha habari ina mapungufu ya kiuandishi, kiuweledi na haiakisi ukweli.