Search
Close this search box.
Africa

Kampuni ya huduma za usafiri kwa njia ya mtandao ya Uber Limited, imetangaza kurudisha huduma zake rasmi baada ya kuisimamisha huduma hiyo tangu Aprili 2021.

Uber Limited ilisitisha huduma zake nchini Tanzania ikipinga kanuni mpya za usafiri wa teksi mtandaoni zilizotangazwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu nchini humo (Latra).

Kwa sasa imetangaza kurejesha huduma zake baada ya kufikia mwafaka na mamlaka hiyo.

Akizungumzia na wanahabari jijini Dar es salaam, Meneja wa Uber Kanda ya Afrika Mashariki, Imran Manji amesema kuwa wanayofuraha kurejea kutoa huduma na kwamba wanaipongeza Serikali kwa juhudi zake katika kukuza sekta ya usafiri wa teksi za mtandaoni.

“Kipaumbele chetu ni kuwa na mfumo ambao utawasaidia madereva kutengeneza kipato cha kujikimu sambamba na kutoa usafiri wa uhakika, wa kutegemewa kwa Watanzania,” amesema Manji.

Manji amezitaja huduma za usafiri walizozirejesha kuwa ni Uber X ambayo amesema kuwa ni huduma ya bei nafuu inayoweza kutumiwa na watu wengi.

Nyingine amezitaja kuwa ni Uber XL, ambayo ni kwa ajili ya wasafiri sita na kwamba magari yanayotoa huduma hiyo yana nafasi inayotoa usafiri wa starehe, inayofaa kwa wasafiri wanafamilia au abiria mwenye mizigo mingi.

Manji amesema kuwa sekta ya usafiri wa teksi mitandaoni imeleta mageuzi makubwa namna watu wanavyoweza kusafiri mijini na kwamba tangu mwaka 2016 Uber ilipoanza kutoa huduma zake jijini Dar es Salaam, imekuwa mshirika kutoa huduma hiyo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Pia amesema kuwa imechangia katika fursa za kiuchumi na kuwapa madereva uhuru wa kufanya kazi kwa muda wanaotaka sambamba na kulipa kodi.

Manji amesema kuwa Uber imeweka msukumo katika usalama na kwamba kwa mujibu wa utafiti uliofanywa (bila kuutaja), abiria wengi hawana uelewa wa vipengele vya usalama ambavyo wanaweza kuvitumia wakiwa safarini.

“Hivyo basi, Uber imeanzisha kampeni ya kuhamasisha kuhusu usalama nchini inayoitwa Safety Chek-Up inayolenga kuhimiza wasafiri kukamilisha wasifu wao wa usalama kwa kuwasha na kutumia vipengele vya usalama vinavyopatikana kwenye mfumo wetu,” amesema Manji.

Amezitaja vipengele hivyo vya usalama kuwa ni kama vile watu unawaamini, uthibitishaji wa PIN na kukagua taarifa za gari na dereva.

“Bila shaka tuna matarajio makubwa ya kesho ya soko la Tanzania na tuko tayari kushirikiana na watunga sera kuimarisha usalama, kusaidia madereva kukuza biashara yao sambamba na kuboresha huduma za usafiri kwa abiria wanaotumia mfumo wetu,” amesisitiza Manji.

Comments are closed