Uganda yakamata mtuhumiwa mkuu wa Utekaji wa Mtalii wa Marekani Mwaka 2019

Serikali ya Uganda imetangaza kukamatwa kwa mtuhumiwa mkuu wa utekaji nyara wa mtalii wa Kimarekani na dereva wake mnamo mwaka 2019 katika Hifadhi ya Taifa ya Malkia Elizabeth.

Kimberly Sue Endicott, raia wa Marekani, pamoja na dereva wake raia wa Uganda walitekwa nyara tarehe 2 Aprili, 2019 na watu wenye silaha waliodai fidia ya dola 500,000 za Kimarekani. Wawili hao waliachiliwa baada ya siku nne kufuatia mazungumzo yaliyoshirikisha maafisa wa Uganda na Marekani. Haikufahamika iwapo fidia hiyo ililipwa.

Msemaji wa jeshi, Meja Kiconco Tabaro, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi vya usalama vya pamoja hatimaye vimefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mkuu, Derrick Memory, ambaye alikuwa mafichoni tangu 2019.

“Memory alikuwa akijificha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako pia alihusika na uhalifu mwingine,” alisema Meja Tabaro. Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa katika wilaya ya Kanungu, magharibi mwa Uganda, tarehe 4 Mei.

“Hii ni hatua kubwa ya mafanikio,” alisema Tabaro, akisisitiza kuwa mamlaka zimejizatiti kuhakikisha usalama wa watalii na wananchi kwa ujumla, na kwamba wale wanaopanga kuvuruga amani ya nchi watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali.

Katika uchunguzi wa awali mwaka 2019, polisi walimkamata Onesmus Byaruhanga, mwenye umri wa miaka 43 wakati huo, kwa tuhuma za kusaidia watekaji. Kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya utekaji nyara na uporaji wa kutumia nguvu.