Uganda yasitisha ushirikiano wa Kijeshi na Ujerumani kwa tuhuma za Uhaini

Jeshi la Uganda (UPDF) limetangaza kusitisha mara moja ushirikiano wa kijeshi na Ujerumani, likimtuhumu Balozi wa Ujerumani nchini humo, Matthias Schauer, kwa kuendesha “shughuli za kihaini” ndani ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Hatua hiyo imekuja baada ya shutuma kutoka kwa maafisa wa jeshi dhidi ya baadhi ya balozi wa nchi za Ulaya kwa madai ya kuwaunga mkono wapinzani wa serikali. Balozi Schauer ametajwa wazi kuwa sehemu ya “mabalozi wanaoendeleza ajenda za usaliti”.

Msemaji wa jeshi, Chris Magezi, aliandika kupitia mtandao wa X (zamani Twitter): “Jeshi la Wananchi wa Uganda (UPDF) limetangaza kusitisha mara moja shughuli zote za kijeshi na ushirikiano wa kiulinzi na Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.”

Tuhuma hizo zimeibuka baada ya taarifa kwamba mabalozi wa Ulaya walieleza wasiwasi wao kuhusu mienendo ya mtoto wa Rais Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mkuu wa majeshi ya nchi hiyo.

Kainerugaba, anayetajwa kuwa mrithi mwenye uwezekano mkubwa wa kumrithi baba yake mwenye umri wa miaka 80, amekuwa maarufu kwa kauli zake tata na vitisho kupitia mitandao ya kijamii. Hivi karibuni, alijigamba mitandaoni kuwa alimteka na kumtesa mlinzi wa kiongozi mkuu wa upinzani kwenye handaki lake binafsi.

Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa X, Kainerugaba aliandika: “Tunayo matatizo fulani na Balozi wa sasa wa Ujerumani nchini Uganda. Tatizo liko kwake binafsi. Hana sifa hata kidogo za kuwa Uganda. Hii haina uhusiano wowote na watu wa Ujerumani, ambao nawaheshimu sana.”

Ripoti za vyombo vya habari vya ndani zinasema kuwa mabalozi hao waliwasilisha malalamiko yao kwa kaka wa Rais Museveni, Jenerali Salim Saleh, wiki hii, ambaye aliahidi kuchukua hatua kumdhibiti Muhoozi.

Hali hii inajiri huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakionya kuhusu kuongezeka kwa ukandamizaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wa serikali kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari, ambapo Rais Museveni anatarajiwa kuwania muhula mwingine baada ya kutawala kwa zaidi ya miaka 40.

Licha ya mvutano huu wa sasa, Ujerumani na Uganda zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu unaotajwa kuwa wa “utulivu na kuaminiana” na thamani ya biashara kati ya nchi hizo ilifikia takriban dola milioni 335 mwaka jana, kwa mujibu wa ubalozi wa Ujerumani, huku Uganda ikiagiza zaidi bidhaa za mitambo na kemikali.

Balozi Matthias Schauer ameihudumia Uganda tangu mwaka 2020.