Uganda imethibitisha kuwa mfungwa mmoja amepata maambukizi ya mpox katika eneo la katikati ya nchi ambalo ni kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo nchini humo.
” tumepata kesi moja iliyo thibitishwa ya mpox katika moja wa magereza yetu, na mgonjwa amezuiliwa na hatua za kudhibiti zimewekwa,” alisema msemaji wa Magereza ya Uganda, Frank Baine.
Baine aliongeza kuwa mfungwa huyo wa kiume alikuwa amekamatwa kwa tuhuma za mauaji na huenda alipatwa na ugonjwa huo kabla ya kupelekwa gerezani katika mji wa Nakasongola, katikati ya Uganda.
Kesi ishirini na moja za mpox zimeripotiwa katika eneo la Nakasongola kati ya jumla ya kesi arobaini na moja nchini kote kufikia tarehe 7 Oktoba, kulingana na wizara ya afya.
Zaidi ya kesi 34,000 zimeripotiwa katika nchi 16 za Afrika tangu mlipuko huu mpya uanze, shirika la afya la Umoja wa Afrika, Africa CDC, lilisema mapema mwezi huu.
Wengi wa kesi hizo zipo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jirani wa magharibi mwa Uganda, ambapo kumekuwa na vifo 988, kulingana na waziri wa afya.
Ugonjwa huu, ambao awali ulijulikana kama monkeypox, unaenea kwa kugusana kwa karibu na watu au wanyama walioambukizwa, ukisababisha homa, maumivu ya misuli na vipele vinavyosumbua kwenye ngozi.
Ugonjwa huu uligunduliwa kwa mara ya kwanza kwenye tumbili mwaka 1958, na unahusiana na virusi vya smallpox ambavyo ni hatari zaidi lakini viliondolewa mwaka 1980.