Ugonjwa wa ajabu waibuka mikoa ya kusini mwa Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema katika mikoa ya kusini mwa Tanzania kumeibuka ugonjwa wa ajabu, ambapo watu wengi wanavuja damu puani mfululizo na kuanguka.

Amesema tayari timu ya wanasayansi na watalaamu wa afya wametumwa kuelekea katika mikoa hiyo hususani Lindi kuchunguza aina hiyo ya ugonjwa, ambao unaweza  kutokana na uharibifu wa mazingira.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimueleza kuhusu ugonjwa huo pindi alipofanya ziara katika mikoa ya kusini.

“Kuna maradhi ambayo huko nyuma hatuyajui, hayakuwepo, lakini kwa sababu tunaharibu misituni, vile viumbe ambavyo vilipaswa vihifadhiwe kule msituni sasa vinasambaa kuja kwa binadamu.

“Kuna kila aina ya maradhi mapya yanazuka ambayo hatuyajui, nilikuwa nazungumza na Waziri Mkuu juzi, ametoka ziara kule mikoa ya Kusini Lindi ananiambia ameona kuna maradhi yameingia wanadamu wanatokwa tu damu za pua wanadondoka.

“Hatujui ni kitu gani wanasayansi, watalaam wa afya wote wamehamia huko wanaangalia ni kitu gani. Kwa nini mwanadamu atokwe tu na damu za pua adondoke, angekuwa mmoja au wawili tungesema ni presha imepanda, vein zimebust anatokwa damu za pua. Lakini ni wengi kwa mfululizo.

“Ni maradhi ambayo hatujawahi kuona na yote ni kwa sababu tunaharibu makazi ya viumbe kule walikoumbwa na Mungu tunawasogeza kwetu wanatuletea maradhi,” amesema Rais Samia.