Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amejiuzulu kama Mwenyekiti wa baraza la Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, akisema wakati umewadia kwa viongozi wapya kuchukua hatamu za kuongoza muungano huo.
Katika waraka ulioandikwa tarehe 5 Oktoba, Uhuru aliwajulisha viongozi wa Azimio la Umoja kuhusu uamuzi huo ambao alidokeza kuwa ulianza kutekelezwa mara moja baada yake kuachia uongozi wa Chama cha Jubilee.
Katika barua ya tarehe 5 Oktoba, Uhuru aliwajulisha viongozi wa Azimio kuhusu uamuzi wake, akisema umeanza kutekelezwa mara moja baada ya kukamilika kwa makabidhiano ya uongozi wa Chama cha Jubilee kwa kiongozi wa sasa Daktari Fred Matiang’i.
Uhuru hata hivyo, alieleza kuwa uamuzi huo haumaanishi kwamba amejitenga na muungano huo au hata safari ya kisiasa iliyoleta vyama tanzu za muungano huo pamoja.
“Uamuzi huu si hatua ya kuondoka katika safari yetu ya pamoja ya kisiasa bali ni hatua muhimu katika kukuza na kuendeleza taasisi za kidemokrasia nchini,” Uhuru alisema.
Uhuru alisisitiza kuwa Azimio si muungano uliobuniwa kwa ajili ya maslahi ya kisiasa bali uliundwa kwa msingi wa kuunganisha sauti za wakenya kutoka maeneo mbalimbali katika juhudi za kulinda demokrasia na maendeleo ya kitaifa.
Akielezea nafasi ya vyama ndani ya Azimio, Uhuru amepigia mfano wa mito midogo inayoungana na kuwa mto mkubwa huku akiweka wazi kuwa vyama vinaweza kuhifadhi utambulisho wao na kushirikiana kuafikia malengo ya pamoja.
Uhuru vilevile amesema moja kati ya majukumu yake kama mwenyekiti wa Azimio lilikuwa kuongoza muungano huo na kuilinda dhidi ya migawanyiko ya ndani.
Ameongeza kuwa uongozi haupaswi kuwa suala la Kung’ang’aniwa milele ila viongozi wanapaswa kuwa na ujasiri wa kuondoka na kuwapa vijana nafasi ya kuendeleza uongozi.
“Uongozi si kung’ang’ania. Ni kuwa na ujasiri wa kujiondoa na kuruhusu kizazi kijacho kupata fursa ya kuongoza safari,” alisema Uhuru.
Hatua hiyo inajiri baada ya Uhuru kukabidhi uongozi wa chama cha Jubilee kwa aliyekuwa Naibu wake Fred Matiang’I, mwezi Septemba. Uhuru alisema wakati huo kuwa ataendelea kuwa mwananchama na mshauri wa chama hicho.
Kujiuzulu kwake kunabadilisha zaidi nafasi yake rasmi katika muungano huo huku Azimio ikiendelea na mchakato wa kuimarisha uongozi wake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.








