Kesi ya uhaini dhidi ya kiongozi wa upinzani nchini Uganda ilianza kusikilizwa Jumanne, wakati serikali ikiendelea na msako mkali dhidi ya mawakili, wanaharakati na vyombo vya habari unaoongozwa na mwana wa rais.
Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwenye umri wa miaka 52, ambaye ni mwana wa Rais na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, katika wiki za hivi karibuni ameagiza kukamatwa kwa wanaharakati mashuhuri, wanasiasa na mawakili. Aidha, ameamuru kufungwa kwa kundi kubwa la vyombo huru vya habari nchini.
Muhoozi anajulikana kwa machapisho yake tata kwenye mitandao ya kijamii, hasa jukwaa la X, ambapo wakati mwingine hujisifu kuwateka na kuwatesa wapinzani wa serikali, na wakati mwingine hutoa utani kuhusu kumuoa mwanamuziki Beyoncé. Mara kadhaa amesema kuwa ndiye atakayemrithi Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ambaye ameiongoza Uganda kwa takriban miaka 40.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema hatua hizi za ukandamizaji zinaonyesha kuwa Muhoozi tayari amekuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini.
Jumanne, mahakama ya Kampala ilianza kusikiliza kesi iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya uhaini dhidi ya kiongozi wa upinzani Dkt. Kizza Besigye, ambaye amekuwa kizuizini tangu alipotekwa nchini Kenya mwaka 2024.
Besigye aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo haiwezi kuendelea hadi pale mawakili wake watakapohakikishiwa usalama wao. Mmoja wa mawakili hao alisema ana hofu ya kutekwa kabla ya kikao kijacho cha mahakama.
“Inaonekana tutashtakiwa tukiwa tumefunikwa macho, tumefungwa mikono na miguu, na tumezibwa midomo,” Besigye aliiambia mahakama.
Wakili mkuu wa zamani wa Besigye, Erias Lukwago, naye alitekwa mwezi huu kwa madai kwamba hatua hiyo ilifanyika kwa maagizo ya Muhoozi. Kupitia mtandao wa X, Muhoozi aliandika kuwa alikuwa “anajivunia maumivu yote nitakayomsababishia.”
Lukwago alitakiwa kufikishwa mahakamani Jumanne akikabiliwa na mashtaka ya kupanga njama dhidi ya serikali, lakini hakuweza kuhudhuria kutokana na hali yake mbaya ya kiafya, hivyo kesi ikaahirishwa.
Wakati huo huo, shirika maarufu la kutetea haki za binadamu la Agora liliitwa na polisi kujibu tuhuma za udanganyifu na utakatishaji fedha.
Hatua hiyo imefuatia uamuzi wa Muhoozi wa kufunga kundi kubwa la vyombo huru vya habari vinavyoendesha gazeti la Daily Monitor na kituo cha televisheni cha NTV, akitangaza kupitia X kuwa: “SIAMINI katika uhuru wa vyombo vya habari!”
Rais Museveni, ambaye alichaguliwa kwa muhula wake wa saba chini ya miezi sita iliyopita, hajatoa tamko lolote kuhusu hatua za hivi karibuni za mwanawe.
Mhadhiri mwandamizi wa Idara ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Makerere, Gerald Walulya, alisema watu wengi hapo awali walikuwa wakiyachukulia matamshi ya Muhoozi kama mzaha.
“Lakini kwa mara ya kwanza sasa tunamuona akionyesha mamlaka makubwa bila kuzuiwa kwa namna yoyote na baba yake,” alisema.
-Mipango ya kumrithi Museveni-
Kwa muda mrefu kumekuwa na tetesi kwamba Museveni alikuwa akimuandaa mwanawe kumrithi madarakani, ingawa jambo hilo halijawahi kuthibitishwa rasmi.
Muhoozi alipata mafunzo katika Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst nchini Uingereza na alipanda vyeo kwa haraka hadi kuwa Mkuu wa Majeshi mwaka 2024.
Amekuwa akieleza mara kwa mara nia yake ya kuwa rais, huku pia akiongoza vuguvugu lake la kisiasa lijulikanalo kama Patriotic League of Uganda.
Katika ujumbe wake wa X mwezi huu aliandika:
“Je, ninyi Waganda mnanipenda? Mtanipigia kura nikigombea baada ya Mzee?”
Hata hivyo, mchambuzi wa siasa na mwandishi wa gazeti la The Observer, Yusuf Serunkuma, anasema hali bado haijaeleweka kwa kuwa Muhoozi anaendelea kusisitiza kuwa anatekeleza maagizo ya baba yake.
Ingawa ana wafuasi wengi mtandaoni, wakiwemo zaidi ya milioni 1.3 kwenye X, kiwango chake halisi cha umaarufu nchini Uganda bado hakijathibitishwa.
“Kama angekuwa na mkakati mzuri, angejifunza kutoka kwa baba yake na kujenga uhusiano mzuri na wananchi pamoja na jumuiya ya kimataifa,” alisema Serunkuma.
“Badala yake, amejitahidi kuvunja uhusiano huo.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Marekani ya Mahusiano ya Nje, Jim Risch, alisema Jumatatu kuwa vitendo vya Muhoozi vinaifanya Uganda kuwa mshirika asiyeaminika, na akataka uhusiano kati ya Marekani na Uganda upitiwe upya.
-Upinzani wazidi kudhoofishwa-
Katika miaka ya hivi karibuni, mpinzani mkuu wa Rais Museveni amekuwa mwanamuziki aliyeingia kwenye siasa Bobi Wine, ambaye aligombea urais mwezi Januari. Hata hivyo, alilazimika kuikimbia Uganda baada ya kupokea vitisho kutoka kwa Muhoozi.
Besigye, mwenye umri wa miaka 70, ambaye amewahi kugombea urais mara kadhaa dhidi ya Museveni, alitekwa mjini Nairobi na watu wenye silaha katika tukio lililolaaniwa kimataifa. Familia yake inadai kuwa amekuwa akiteswa akiwa kizuizini.
Wakili wake, Erias Lukwago, alikuwa akijiandaa kuwasilisha hati za kisheria zinazomtaka Muhoozi afike mahakamani kujibu tuhuma za utekaji wa Besigye, kabla ya yeye mwenyewe kukamatwa mwezi huu.