Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Busara Promotions nchini Tanzania,Yusuf Mahmoud, ametangaza kusitisha kwa shughuli zinazofanywa Busara Promotion za kusheherekea utamaduni na muziki wa Kiafrika linalojulikana sana kama Sauti za Busara, ifikapo Machi 31,2022, kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha.
Pazia la Sauti la Sauti za Busara linafungwa ikiwa ni baada ya takribani miaka 19 tangu lianze ambapo limekuwa likiwakutanisha wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Machi 24, 2022, Mjini Unguja, bwana Yusuf Mahmoud, amesema bila fedha za kulipa gharama za ofisi au mishahara tamasha hilo haliwezi kuendelea tena.
Tamasha la Sauti za Busara limeanzishwa Machi 2003, moja ya tamasha linazoongoza barani Afrika kwa kutangaza na kusherehekea muziki na urithi wa kitamaduni wa Afrika.
“Wenyeji wengi watakumbuka jinsi tamasha lilivyoubadilisha mwezi wa Februari kutoka msimu wa chini ya wageni 3,000 waliotembelea Zanzibar mwaka 2004, hadi kufikia zaidi ya wageni 40, 000 kwa mwezi huohuo kabla ya ugonjwa wa Uviko 19,” amesema
Hata hivyo, Mahmoud amesema hayo yote yasingewezekana bila msaada wa wahisani, wafadhili na washirika hususani ubalozi wa Norway nchini Tanzania ambao ulitoa ufadhili wa kuendesha shirika ili kuendeleza na kutekeleza mipango mkakati wake kuanzia Oktoba 2009 hadi Machi 2022.
“Usaidizi wa kifedha wa Norway umefikia mwisho wake mwaka huu, kwa hiyo bila ufadhili mwingine wa sekta ya umma au binafsi, busara promotions haiwezi kuendelea kuwapo,” amesema
Meneja wa fedha na utawala, Safina Juma amesema tofauti na matamasha mengine hilo liliangazia muziki wa moja kwa moja wenye utambulisho wa kipekee huku vipaumbele vyake vikiwa kuwapa nafasi wasanii wa kike, wasanii wapya na chipukizi.
Amesema kwa mwaka wanatumia dola za Marekani 120,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 278 kwa ajili ya kuendesha ofisi pekee.
“Kwa miaka mingi tamasha limekuwa nguzo ya mfumo wa ikolojia ya muziki wa Afrika Mashariki, likitoa ajira, kukuza biashara, kutoa mafunzo na kukuza ujuzi,” amesema Safina